Tuesday, December 11, 2012

WEWE INGIA KULIA, WEWE NENDA KUSHOTO



    WEWE PITA UINGIE KUSHOTO UNASTAHILI, WEWE PITA UINGIE KULIA UNASTAHILI !!!


Hii itakuwa ni amri ambayo haitakuwa na mjadala,ujanja ujanja, ubaunsa wa kupitiliza kuwazidi malaika wa Mungu na Mungu mwenyewe kama vile ilivyo ngumu kuzuia kifo basi katika tukio hili kutakuwa hamna ujanja ujanja.
Kipindi cha Nuhu watu au binadamu wa wakati ule waliambiwa watengeneze njia zao kwa kumrudia Mungu lakini walimuona Nuhu kuwa kama amechanganyikiwa, hana pesa,mlokole, hajasoma, masikini mkubwa, wengine walimtukana, wakawa wakiendelea kuponda starehe wengine wakijenga majumba kila kukicha. Ndivyo ilivyo hata leo injili inahubiriwa karibu kila kona ya dunia mahospitalini, vituoni mwa dala dala, katika maeneo ya wazi, lakini matokeo yake wahubiri hawa huishia kutukanwa, kuonekana kuwa kama wamechanganyikiwa na dini, hawana pesa,hawana elimu ya kutosha, wamekosa kazi za kufanya.

 

Watu wa kizazi kile cha Nuhu walitegemea ujuzi wao wa kuogelea, baada ya kuambiwa jamani tumrudie Mungu kwani tusipomrudia tutaangamizwa kwa mvua kubwa, ah! Wapi siku ya siku walioweza kuogelea walijitahidi mpaka katika mlango wa safina, lakini mlango haukuweza kufunguka maana aliye funga mlango alikuwa ni Mungu mwenyewe (Mwanzo 7:16).Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyoamuru Mungu; Bwana akamfungia.
Mungu katika maandiko yake amesema sitaiadhibu dunia tena kwa maji (Mwanzo 8:21) Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitaipiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Mungu anaposema sitaadhibu tena kwa maji maana yake adhabu ipo, Mungu ni wa nuruni hakuficha katika sehemu nyingine katika maandiko yake amefunua wazi adhabu itakuwa ya namna gani (Marko 9:43-48) Na mkono wako ukikukosesha,ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu kuliko, kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanam, kwenye moto usiozimika; (ambao humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki) Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanam; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.


 


Pia tunamuona Mungu akiwaagiza Adam na Eva wasile tunda katika katika mti wa katikati ya bustani hapa Mungu alikuwa anaagiza kwamba wasifanye dhambi ila watii sheria ili waende sawa, ila tunamuona shetani (Nyoka) aliyejaa hila na udanganyifu akiwapotosha ili watu hawa wamkosee Mungu wasifikie malengo ambayo Mungu alikuwa amewawekea, kama alivyofanya hila kipindi cha wazazi wetu (Adam na Eva ) wakakosea ndiyo hila hiyo hiyo anayoitumia katika kizazi hiki kwa kuleta dini na madhehebu lukuki mengine ya uongo na mengine ya ukweli na watumishi wa Mungu ambao wengine sio bali ni wa Shetani, ila wanavaa mavazi ya kondoo, bila msaada wa Roho mtakatifu ni ngumu kuwatambua maana na wao wanaitumia biblia hii takatifu,na wanafanya miujiza kwa jina la yesu, ila hawamtaji yesu yupi, katika biblia kuna yesu wengi (Matendo 13:7) Walipopita katikati ya kisiwa chote mpaka pafo, wakaona mtu mmoja,mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu. ndio maana wakati Yesu alipokuwa akiondoka alituachia Roho Mtakatifu bila huyo sijui ingekuwaje! maana hawa watu wanaojiita watumishi wa Mungu si wa Mungu ila ni wa mungu wa dunia hii (2 Wakorinto 4:4) Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.


Sisi je! Tutapataje kupona tusipojali wokovu mkuu namna hii bila kumkimbilia Yesu (Waebrania 2:3) Sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia.  ambaye peke yake ndie mwenye uwezo wa kutufikisha kwa Mungu na sio mwingine yeyote awe nabii aumtume au kuhani au mwalimu au profesa au mtabiri ambaye akifa ni kuoza tu. (Matendo 4:12).Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

Baada ya Wazazi wetu kufanya kosa kila mmoja alipata adhabu yake nyoka kutembea kwa tumbo, mwanamke kuzaa kwa uchungu na mwanamme kula kwa jasho lake sababu yeye Mungu hana upendeleo kila mtu atahukumiwa kutokana na matendo yake.
Nini maana ya dini, dini ni mpango wa mwanadamu wa kumtafuta Mungu au mungu uamuzi ni wake binafsi.

 

Wokovu ni mpango wa Mungu wa kumtafuta mwanadamu ili aje katika kusudi lake (Yoh 3:16) Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Wewe upo njia ipi? Duniani hapa njia zipo nyingi mpaka mtu unaweza kuchanganyikiwa njia za Mungu wa kweli na mungu wa uongo humo humo ni michanganyo tu, ni kipindi ambacho Yesu alitabiri juu yake akisema siku za mwisho aliposema, nyakati za mwisho kutatokea makristo na manabii wengi wa uongo. (Mathayo mt 24:11) Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi
Kama ilivyo kwa Mungu kwa kuwa anazo nguvu na shetani naye anavyo vi guvu, kila upande unamvuta mwanadamu aje kwake, hapa sasa itategemea hiyari ya huyo mtu anayetakiwa na kila upande.Mungu ndiye muumbaji ana uchungu na watu wake ndio maana kwa gharama yeyote anawaangaikia, twende kwake ili tupate uponyaji, shetani yeye hana uchungu anasubiria hukumu, kiboko chake na kila siku anajitahidi watu waje kwake ili kuongeza idadi ya wafuasi ambao ataenda nao motoni, ingawa ule moto ni kwa ajili ya shetani na malaika zake binadamu ataingia katika janga hili kwa kujitakia tu (Mathayo 25:41) tena wakati mwingine akikisia huyu anataka kuniacha anaweza akamuondoa duniani halaka halaka ili akose nafasi ya kutubu kabisa awe anasubiria hukumu tu, sababu shetani anajua ukisha maliza kifo utakuwa unasubiria hukumu tu, pia anawatajilisha kwa utajili huu wa duniani ambao una mwisho unatajirika kwa kuwa ana kila kitu cha hapa duniani, ila mambo ya mbinguni hata a,e,i,o,u yake hujui.
Mitume, manabii, walimu, maprofesa, wachungaji wote waliokwisha kufa wamekufa nao wanasubulia hukumu yao siku ya mwisho kama walifundisha uongo watapata malipizo yao na adhabu ya milele kwa moto wa jehanam na kama walifundisha mema watapata thawabu yao, kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake au kila mtu atavuna kile alichopanda. Na Yesu ndiye atakaye rudi siku ya mwisho si mwingine yeyote, wote wamelala mpaka siku ya mwisho, hapo ndio itakuwa ni kizaa zaa hakuta kuwa na muda tena wa kusikia habari za injili neema itakuwa imefungwa, maana sasa hivi neema hii ipo wazi, imefunuliwa kwa watu wote, kuna muda unakuja itafunikwa, itapigwa stop. (Tito 2:11) Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa.  Sijui itakuwa vipi ndugu yangu, je utaamua kesho ? unajua ya kesho wewe Mungu amekupangia nini? (Mithali 27:1) Usijisifu kwa ajili ya kesho; kwa maana hujui yatakayo zaliwa na siku moja.
Unaweza kujiuliza hivi, hivi kwa nini Mungu asingeruhusu watu wapenye yaani waende bure bure tu, Mungu hana upendeleo kwa Yesu ukombozi ulimghalimu nawe pia lazima uchangie gharama,sababu wewe upo upande wa Mungu yeye alichangia, Yesu alichangia, Roho Mtakatifu alichangia kwa nini wewe usichangie? hujui kuwa uliumbwa kwa mfano wa Mungu ?na vile vile Mungu hapendi watu wapate kitu bure bure, hata Adamu na Eva Mungu aliwapa bustani/shamba walime, alikuwa na uwezo wa kuwapa chakula bure, ila si utaratibu wa Mungu kupata kitu bura bure tu, ukienda kinyume na maagizo yake utakuwa unamtenda dhambi, pia Mungu hana upendeleo. Mungu hataki watu wavivu anataka kila kitu ukifanyie kazi, aliumba dunia kwa siku sita siku ya saba akapumzika wewe ni nani usiye taka kufanya kazi, Kama Mungu alivyo nasi pia tupo hivyo hivyo.
Mungu ni mpole sana, tena ni mkali sana, tena anatupenda sana, tena ana hasira sana juu yao wote watendao mambo maasi, hacheki na dhambi Mungu anaangalia neno lake apate kulitimiza, haendi kinyume na alivyosema pia hana kigeu geu, ikiwa alisema atatimiza. Kama alisema Yesu atarudi mara ya pili atarudi kweli si uongo, hata kama atachelewa atarudi.

 

Mungu anapoona mtu yeyote hata kama anatoa sadaka sana, anasali sana ana huruma sana haisaidii sana kukufanya uwe na sifa ya kwenda mbinguni kwake, lazima umkiri huyu Yesu upate msamaha na ondoleo la dhambi uwe na tiketi ya kumuona mwokozi, vinginevyo siku ya siku utaishia wewe pia pita huko kushoto unasthahili, malaika wakikusindikiza bila kuwa na la kujitetea.
Kama utahitaji kuepuka balaa hilo, la kuikosa mbingu ambapo hata viongozi wetu wa dini nao watakuwa wanasubiri katika zamu zao wakisubiri mishahara yao hawataweza kumtetea mtu awaye yote. Watasimama mbele za Mungu wakitoa hesabu ya matendo yao (Warumi 14:12) Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.
Mbegu hupandwa ikafa na kuleta mmea mwingine mpya mzuri, ndivyo hivyo miili yetu ya udongo itakuwa ilisha kufa na kuoza na kuinuliwa tukiwa na miili mingine ya kiroho au ya kimbingu mbingu.
Kama utapenda kujiunga na wanao mwamini Yesu tafuta mahali palipo tulia na kufuatisha maneno ya sala hii iliyoandikwa, uisome kwa kumaanisha baada ya kumaliza maneno ya sala hii utakuwa umemkaribisha Yesu ndani ya moyo wako naye atakuwa wako (Warumi 10:9) Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.  pia hata kuacha mpaka mwisho wa dunia, ila pia kama hutakuwa tayari ni wewe mwenyewe sasa maana wokovu kumwamini Yesu si lazima ni hiyari, maana Mungu humpenda yeye afanyaye mambo yake bila kulazimishwa.(2Wakoritho 9:7)
Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye (moyo) kwa moyo wa ukunjufu.

SALA 

“Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha.....(zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa na unijaze na Roho wako Mtakatifu aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu kwa kuniokoa.” Amen

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha, basi utakuwa umeshakombolewa, umeokoka.Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili kusonga mbele.


1. Soma Neno la Mungu biblia takatifu kila siku (Warumi 10:17),  (Wakolosai 3:16)
2. Sali asubuhi mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1Wathesalonike 5:17)
3. Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokiri wokovu        na kutoa mafundisho ya kiroho upate kuukulia wokovu. (1Petro 2:1-2), (Waebrania 10:25).
4. Usikubari kusikiliza uongo wa Shetani (Ufu 3:11), (Mwanzo 3:1-19 )na (1Petro 5:8)
5. Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo, na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani anahitaji          ujumbe kama huu siku hii ya leo.(Ufunuo 22:18) , (Kolosai 4:16).


                            Ni mimi


               Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
                injiliyajioni@gmail.com
                www.injilijioni.blogsport.com

 





1 comment:

  1. Safi, nimeipenda, Ubarikiwe mtumishi wa Bwana

    ReplyDelete