Tuesday, August 30, 2022

MLANGO WA MBINGUNI

 






Mlango ni njia ya kuingia mahali na kutokea

Katika miji kawaida kuna kuwa na milango ya miji kwa ajili ya usalama wa mji husika, hata katika Israeli kulikuwa na ukuta na inasemekana kuna milango 12, na Bwana Yesu katika utumishi wake hapa duniani alikuwa na mitume 12, pamoja na mmoja kukengeuka akamweka mwingine aliye chukua nafasi ya Yuda Iskariote anayeitwa Mathiya.

Dini au Madhehebu ni mpango wa mwanadamu kumtafuta Mungu na Wokovu ni mpango wa Mungu kumtafuta mwanadamu.

Dhambi ya Adamu na Hawa ilipelekea dunia yote kuwa chini ya Shetani na shetani akawa ndio  mungu wa dunia hii, (2Wakorintho 4:4 Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasio amini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.) mungu si ndio anayeamua nini kifanyike katika dunia, Shetani huamua ajari itokee, maafa yatokee na kweli huwa  yanatokea. Wakati mwingine neema huweza tokea yakazuiwa katika maombi siri hii wanayo baadhi ya walokole ambao wanadharaulika katika jamii wanaonekana kama wamechanganyikiwa au hawana elimu, au pesa. si kila mtu aliyeokoka anaweza badilisha tukio wengine ni walokole feki, kwa hiyo tukio baya linageuzwa na kuwa jambo jema na Mungu anajipatia utukufu (Yeremia 1:10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa na kuharibu na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.) maana shetani hutuwazia mabaya kila siku na yeye kazi yake ni kuua kuharibu. (Yohana Mtakatifu 10:10 Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu ; mimi nalikuja ili wawe na uzima , kisha wawe nao tele.)

Leo hii kuna dini lukuki wengine wanasali Jpili, Jmosi,Jtatu kila mmoja anadai siku yake ndio sahihi, wengine wanaabudu na kujitumainisha kuwa siku wakifa watamiliki majengo na magari na kuishi kama paradiso, hapa hapa duniani wengine wanamuabudu mama na kudharau mtoto, wanakuambia mtoto na mama bora mama, mtoto Yesu hana kitu Makanisa ya mashetani yapo wazi wala siku hizi sio kificho na wanatafuta waumini kwa bidii kweli, Mbeya kuna kuna kanisa wanaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja na kunywa pombe tani yako na wana maandiko ya kusimamia, kuoa mke zaidi ya mmoja ruksa Mbona Yakobo alioa au Daudi, Yakobo walioa kwa hiyo ruksa. Ukifuatilia madhehebu ni mkorogano mtupu unaweza kuchanganyikiwa twende kanisa gani lipo sahihi maana kila kanisa linadai lenyewe ndio sahihi kuliko lingine, kuna siku nilienda kanisa la Nabii mmoja anafanya miujiza miujiza akawa ana jock makanisa mengine anasema njoo huku umwone mungu live achana na makanisa mengine ambako mungu wao amelala.

(Yoh 10: 9 Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.) Yesu anasema yeye ndiye mlango hivyo akili zetu zinajua mlango wa kuingia mahali na kutoka katika uumbaji mlango hauna maana ya kitu bali mtu ndio maana Yesu anasema  ‘mimi ni mlango’ haina maana tunafungua mdomo au kinywa chake tunaingia tumboni mwake , ni mtu anayeweza kufanya jambo fulani na kusababisha jambo kutokea.

(Mathayo 16:18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda, milango ya kuzimu ni mapepo)

Kama vile ambavyo mtu anakuwa na ratiba zake kwa siku au kwa mwaka naye Mungu ana ratiba zake ni kweli lango lipo wazi kuna muda hili lango litafungwa halitafunguliwa ngo.

Kuna wimbo wa Kikristo unasema LIPO LANGO MOJA WAZI NI LANGO LA MBINGUNI

(Luka mt 9:23 – 24 Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe ajitwike msaraba wake kila siku, na anifuate.Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza , na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.)

Ndo maana hata wanafunzi wa Yesu karibu wote vifo vyao vilikuwa ni vya mateso sana ili kusudi wakate tamaa waachane na Yesu wapotee milele, Petro alisurubiwa katika msaraba uliogeuzwa kinyume na ule wa Yesu, Yohana alitupwa kwenye pipa la lami inayochemka akawa hafi mwishowe wakamtupa kwenye kisiwa cha patmos, huko akaja kuandika kitabu cha ufunuo, Tomaso alipigwa mshale alipokuwa ameenda katika shughuli za kimisionari huko India, Paulo ni mtume aliyefungwa muda mrefu gerezani pia huko akawa akiandika nyaraka vitabu mbali mbali baadaye alichinjwa. Stefano alipigwa kwa mawe hadi akafa. Kwa hiyo ugumu wa njia hii walioupitia wenzetu ndo nasi tunapitia ukitaka mteremko basi safari yako mwisho wake ni mbaya. Utachukiwa na dunia na shetani pia (Luka mt 10:23 “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu, lakini mwenye kuvumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka”)

Pia mtumishi Adam haji Aliyeokokea Somalia ameshuhudia mahali alipoamua kumuoa msichana mmoja na huyo msichana alipoamua kuokoka aliingizwa kisu katika uke wake na kuinuliwa juu na kupasuliwa katikati na kufa hapo hapo.

Yesu ametoa tahadhali njia ya mbinguni sio lele mama ina vita vikali, Shetani anapambana na wote ili kuwakatisha tamaa waishie njiani warudi nyuma ili wakosee nao waingie mlango wa kuzimu alioandaliwa Shetani na Malaika zake mwanadamu ataingia huku kwa kutojari au kutowasikiza akina Musa na manabii kama tahadhari, kama yule tajiri aliyeingia motoni na kutamani kurudi duniani japo dakika moja haikuwezekana.

Yule bwana mjinga likwenda bila cheti, Mbinguni watu hawaingii kiholela holela tu kuna utaratibu ndo maana utakuta sehemu nyingine katika mifano ya Bwana Yesu ametumia kama siku ya harusi ya mwanakondoo, yaani kuingia hapo ni kwa watu maalumu wenye cheti yaani Wokovu bila hicho njia nyeupe nenda kuleeee mbali motoni kilio na kusaga meno milele.

(Zaburi 118: 20 Lango hili ni la BWANA, Wenye haki ndio wataoliingia.)

Haki tunaipata baada ya kumkiri Kristo Mwana wa Mungu aliye hai pekee, usipomkiri, ukikata basi ujue hukumu inakusubiri na moto wa jehanamu unao tamani upate chakula chake, yaani watu wasiomkiri Yesu katika kipindi hiki cha neema kabla lango halijafungwa, likifungwa halitafunguliwa ng'o milele.

Ukikosa sifa za kuingia katika lango la mbinguni basi wewe utakuwa na sifa za kuingia katika mlango wa kuzimu utapokelewa na wenyeji wa huko kwa ajili ya mateso ya milele pamoja na shetani, tuamue leo watu wengi hawajamkiri Kristo wanajifariji kuwa wataingia mbinguni kwa sababu wanaimba kwaya au wanatumika madhabahuni, wamepata komunio, kipaimara, mbinguni watu unaingia kwa kumkiri Yesu kwa kinywa chako mwenyewe (Warumi 10:9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa ni Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.) Kumwamini Yesu ni hiyari hakuna anayelazimishwa kuamua hivyo kwa sababu karibu mambo mengi ya Mungu tunatakiwa tufanye kwa hiyari kwa moyo wa kupenda bila kulazimishwa, ila ndo hivyo ukikubari utakula mema ya nchi ukikataa basi hukumu inakusubiri.

Kutokubali kumkiri Yesu ni kutokubariana na Mungu uamuzi wake wa kumtoa Yesu afe msarabani na kutulipia deni na badala yake unakuwa upo tayari kulilipa mwenyewe bila msaada wa Mungu, na ili kulilipa hili deni ni kuingia katika moto wa milele pamoja na Shetani yaani tunakuwa tunaona kama vile Shetani ameonewa bora twende motoni wote, ingawa ule moto Mungu aliuandaa kwa ajili ya Shetani na malaika zake.(Mathayo mt 25:41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na  malaika zake.) Binadamu ataingia kwa kujitakia mwenyewe. Kwa sababu binadamu yeyote aliye hai Duniani leo ana maamuzi ya kuchagua kwa hiyari yake mwenyewe njia aitakayo aende motoni au mbinguni? baada ya kufa hakuna nafasi hiyo tena. Kama yupo mtu yeyote anatumainia baba au babu ni kiongozi mkubwa sana wa dini akuombee sala nzito ya kuwekwa mahali pema peponi ni uongo wa mchana kweupeee. Mungu hana kigeu geu (Malaki 3:6  Kwa kuwa mimi; BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo) 

Pia kama utatangulia mbele ya haki ndo neema yako itakuwa imeishia hapo, sababu maandiko yanasema baada ya kifo kinachofuata ni hukumu. (Waebrania 9: 27 – 28 27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; 28 kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtamiao kwa wokovu.)

Kuna watu wengi wataingia motoni kwa kudhani  kuwa baba au mama walikuwa ni Wakristo basi automatic na wao ni wakristo hivyo mlango wa mbinguni ni halali yao haipo hivo dini sio kabila.Mahusiano ya mtu au binadamu na Mungu wake ni ya binafsi mtu na Mungu wake sio kufuata mkumbo, kurithi. Na kila mtu atasimama mbele za Mungu kueleza habari zake (Warumi 14:12 Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.) Wengine katika kanisa huenda wanafanya huduma za madhabahuni mf. Uzee wa kanisa , Ushemasi, kuongoza sifa, Kuomba na hata kutoa mapepo hivyo vyote sio tiketi ya kuingia Mbinguni, Mbinguni tunaingia kwa tiketi moja tu ya wokovu, unao patikana kwa Yesu pekee sio mtu yeyote Maria, Petro, Muhamedi, Zumaridi, Paulo au mtume yeyote aliyepo au atakayekuja na kufanya miujiza kabambe. (Matendo ya mitume 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.)

Mungu hana upendeleo anatupenda binadamu wote na pia anatuwazia mema, ila hapo hapo Shetani hatuwazii mema anatamani watu wote duniani tuikose mbingu, twende motoni pamoja naye kwa hiyo binadamu tunatakiwa tujiongeze, tujue lengo la Mungu na lengo la Shetani na kufanya uamuzi wa kuchagua,Yoshua 24: 15 Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakaye mtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. (2 Wakorintho 6:2 Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia ; tazama, Wakati ulikoubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndio sasa.) Tuchague leo, sio kesho, hatujui kesho yako, Amina Barikiwa.

Kama utakuwa tayari kwa ajili ya maamuzi haya muhimu ambayo yatakusaidia sasa na hapo baadaye, tafuta mahali pa utulivu na usali sala ifuatayo iliyoandikwa ukimaanisha, baada ya sala tu utakuwa umesha mpokea huyu Yesu, na atakuwa Bwana na Mwokozi kwako sasa na milele.


“Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha, niwezeshe kutozirudia kabisa na unijaze na Roho wako Mtakatifu aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu kwa kuniokoa.Amen”


Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha, basi utakuwa umeshakombolewa, umeokoka.Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili kusonga mbele.

1. Soma Neno la Mungu biblia takatifu kila siku. (Warumi 10:17), (Wakolosai 3:16)

2. Sali asubuhi mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1Wathesalonike   5:17)

3. Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokiri  wokovu na      kutoa mafundisho ya kiroho upate kuukulia wokovu. (1Petro 2:1-2), (Waebrania 10:25)

4.  Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo,   (2Thesalonike                       3:10)

5. Usikubari kusikiliza uongo wa Shetani. (Ufunuo 3:11), ( Mwanzo 3:1-19) (1Petro 5:8)

6. Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo, na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo.(Ufunuo 22:18) ,( Kolosai 4:16)


                                                                               Ni mimi 

Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
injiliyajioni@gmail.com
www.injilijioni.blogsport.com




 

2 comments: