(Mathayo Mtakatifu 24:11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi).
Neno la Mungu lipo wazi limetahadharisha kutokea kwa Manabii wengi wa uongo na kudanganya wengi, sio manabii tu, wachungaji, watu wa maombezi, Watumishi wa Mungu,Wahubiri, makuhani, Maaskofu, Mitume, Waalimu hizi ni nyakati za kukaa vizuri na Mungu wako pia si wakati wa kuwa vugu vugu ni heri uwe moto au baridi, ukiwa vugu vugu ni rahisi sana kusombwa na mafuriko. (Ufunuo wa Yohana 3:15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto). Hizi ni siku za Mwisho kila mtu anatakiwa awe makini na awe macho kweli kama wateule wameambiwa wawe macho, itakuwaje kwa watu wasio wateule?
(Mathayo Mtakatifu 24:24 Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.)
Cha ajabu hawa wanaojiita watumishi wa Mungu kwa matendo yao si watumishi wa Mungu aliye hai, maana kama wanaombea watu walioumbwa na Mungu na kuwadai POSHO KUBWA KUBWA tuwaulize kwa andiko lipi au ni lini Yesu aliombea mtu, au mitume wapi waliwahi kuombea mtu wakadai posho, na kama mtu hakutoa posho hakupata maombi aliyostahili.Kuweka posho kidogo ya wastani mfano ;5000/= au 10,000/=(kwa huduma changa, ila huduma ikiwa imekua inaweza kuwekwa kikapu na watu wakawa wakichanga kwa jinsi ya watakavyoguswa sio mbaya ili kuiwezesha huduma kukua, kununua au kukarabati viti vya huduma, kumuwezesha mtumishi naye kama binadamu aweze kukidhi mahitaji ya familia yake naye ana watoto, mke au mume ,kulipia TRA vibali n.k, kulipia umeme,kulipia maji, mtumishi naye anatakiwa avae vizuri yeye na familia yake ila kucharge gharama ya 200,000/= au 300,000/= kumuona mtumishi tu, haijakaa sawa. Maisha ya siku hizi sio kama ya zamani siku hizi kila kitu pesa, huwezi sema unaenda alummiun Africa kampuni ya mabati ukaombe bati kwa ajili ya kuwezesha wahitaji wakae pazuri, Au uende kampuni ya Bakresa ukaombe akupatie maji ya bure kwa ajili ya washirika wako, hiyo kitu haiwezekani (Mathayo Mt 10:8 Pozeni wagonjwa, fufueni wafu,takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure). Kuna jumbe Yesu aliwaambia wanafunzi wake kipindi kile kutokana na mazingira ya wakati ule ilikuwa sahihi, ila kwa mazingira ya sasa tuliyonayo inabidi kujiongeza. Kumalizia kipande hicho kuna sehemu imeandikwa Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Jiulize unaweza kwenda benki bila utaratibu ukachukue mi hela kwa sababu ni mali ya BWANA?
Kama tunatakiwa kulipia Mungu angetuambia tulipie pumzi ya uhai ni tajiri yupi leo angeliweza kulipia? Ulizia wagonjwa wanaolazwa na kuhitajika wawekewe oxygen gharama yake ni kubwa mno unaweza kuta lisaa limoja gharama yake inaweza zidi hata milion moja, Mungu wetu Muumba wa mbingu na nchi anatufanyia vitu vingi mno bure kabisa Ulinzi, Uhai, pumzi, Amani, uwezo wa kuongea, kusikia, viungo vya miili yetu vilivyo ndani ya mwili na vilivyo nje ya mwili kufanya kazi yake ipasayo vizuri tu, hatulipii kutokana na makosa yetu, anatuwazia mema siku zote (Yeremia 29:11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi.Asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu)
Mbona wengine wanamkosea Mungu na Mungu aliye hai hawaadhibu?, anawaacha tu, Mungu wetu mkuu ni mpole sana lakini pia ni mkali sana, kwa hiyo ni lazima tumpende tumuheshimu na pia tufate maagizo na miongozo yake. Bila yake yeye hatuwezi kumshinda huyu mwovu shetani , kwani shetani ana nguvu zaidi yetu pasipo msaada wake Mungu. Mungu hamlazimishi mtu yeyote kumfuata yeye, alishaongea mara nyingi kwa kutumia vinywa vya watumishi wake mbali mbali akitaka wote tumfuate Yesu ili tupone, tuokoke. Hatutaki? Je unataka ashuke toka Mbinguni mwenyewe ili wewe ufanye maamuzi ya kuokoka' kumkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi? Sasa kwa taarifa yako Mungu hatashuka Ng'o ili kukushawishi wewe umwamini Ukikubari umepona na ukikataa hukumu ya milele inakusubiri.Chaguo ni lako binafsi kumfuta Yesu au wengine unaowajua na kuwaamini wewe.
Ingawa Mtumishi wa Mungu hupimwa kwa matendo, lakini haijalishi mtumishi anafanya wema fulani mf.kutoa pesa, kusaidia wahitaji,anaponya wagonjwa, anatenda miujiza, anafufua wafu, anatoa mapepo, anafukuza wachawi, hatumpimi mtumishi wa Mungu kwa jambo moja tu au mawili, lazima tumkague kwa mambo mengine pia ili aweze kufaulu mtihani, hata maandiko yametuasa kuwa tusiziamini kila roho bali tuzijaribu , maana manabii wengi wa uongo walitokea, wametokea na watatokea.
(1Yohana Wapenzi, msiimini kila roho, bari zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.)
Viroja/Vituko vya manabii wa uongo
1. Ukilipa fedha nyingi unaombewa sana ukitoa kidogo unaombewa kidogo, kwa lugha nyingine kwenye nyumba za ibada hizi matajiri wanaombewa zaidi kuliko masikini.
2. Manabii wa uongo hawa wanatumia chumvi, sabuni, pete maalum,bangili, cheni, mafuta, maji, stika, picha zao binafsi vyote hivyo sio bure bure.
3. Baadhi ya hawa manabii wanataka waabudiwe, wasujudiwe sifa ambazo anayestahili kuzipata ni Mungu peke yake.
4. Baadhi ya hawa mitume hawa wa uongo wanashika viungo nyeti vya baadhi ya akina mama ambao ni wake za watu wanaopitia changamoto mbali mbali katika maisha. Mf.kukosa watoto, kutokuwa na kazi. Wanajifananisha na Madaktari wa kawaida ambao wakati mwingine huweza kumkagua mgonjwa, sehemu mbali mbali za mwili wake ili kumuondolea, kujua shida fulani inayomsibu.
5. Baadhi ya watumishi hao manabii wanasumbua wafuasi wao wakisema kwa kuwa wao ni watakatifu waliopo duniani kwa hiyo hawapaswi kukanyaga adhi iliyo jaa dhambi.Kwa hiyo wabebwe wanapohubiri na wanapoombea wagonjwa.
6. Kwenye makanisa ya nchi za jirani waumini wanachapwa viboko kama njia mojawapo ya kutoa mapepo. Huko huko kuna baadhi ya watumishi wanasumbua waumini wao wakitaka wanunuliwe magari ya kifahari sana kwa kuwa Mungu ni tajiri. Sehemu nyingine waumini walifungiwa milango, taa zikazimwa mahekaru yakachomwa moto maelfu ya watu wakafa.
7. Kuna mwingine namjua, kwa macho nimemwona alikuwa ana agua kwa kutumia mizimu, ila hivi karibuni nilionana naye tena mwenyewe kabisa akaniambia sasa hivi anaendelea na kuagua ila anatumia biblia.Na wateja, waumini lukuki kila siku jioni anawaombea wagonjwa, pia anawaza kupanua wigo wa huduma yake maana wateja wamekuwa wengi mno.
8. Uwe makini sana na mjuzi wa neno la Mungu ukisaidiwa na Roho Mtakatifu bila hivyo ni ngumu kuwatambua, ukifika kwenye makanisa yao utakuta nao wanataja taja kuwa siku hizi kuna manabii wa uongo wengi tuwe makini sana.
9. Wanapoombea wagonjwa, wateja wao baadhi ya hawa watumishi huwakanyaga wahitaji au wenye shida au kuwachapa fimbo kama njia moja wapo ya kuagua au kutoa mapepo na majini.
10. Huweza hata kudhalilisha muumini anaye muombea mfano: Kumdhalilisha muumini au mteja mwenye tatizo la kukojoa kitandani kwa kusema wewe unakojoa kitandani hadharani, wakati kwa hekima tu ungeweza kumfanyia kwa faragha, ili kumlinda mteja na sio hivyo mnamdhalisha na wewe kubeba sifa na utukufu.
Kila kukicha watumishi wapya na mafunuo mapya wanazuka, na style zao za kiutumishi na style zao za maombezi inayowapelekea watu kuzubaa na kubweteka katika kutegemea maombi ya watumishi kila siku wakati suala ala maombi ni jambo linalomwusu kila muumini. Kama maandiko yanavyosisitiza tusikome kuomba na sio tusikome kuombewa. (1the 5:17 ombeni bila kukoma;)
Maandiko yapo wazi yakisema ole wake wa yule apotoshaye, anayesababisha makwazo (Luk 17:1 Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake !)
Sio kweli kuwa manabii, watumishi wa kweli hawapo ila katika watumishi hao hao wengine ni wa uongo, na changamoto iliyopo ni asilimia kubwa ya watu hawana muda wa kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kusoma na kuelewa, neno la Mungu hivyo basi inapelekea watu wengi kujikuta wameingia kwenye mkumbo wa Manabii,watumishi hao wa uongo. Na maandiko yapo wazi hayakupepesa macho kwa habari ya tahadhari, maandiko yameonya kuwa. Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.)
Hawa watumishi wa uongo yote wanayoyafanya wanaongozwa na babayao aliye baba wa uongo (Yohana Mt 8:44 Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa ya baba yenu ndio ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa ni mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na babaa wa huo.)
Ukimfuata shetani na kumtumikia siku ya mwisho itakapofika utahukumiwa pamoja naye katika ziwa la moto, maandiko yapo wazi (Mathayo Mt Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto,Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari ibilisi na malaika zake;)
Wewe unamfuata nani? nani mwanzilishi wa imani yako sasa kwa taarifa yako kule alikoenda, alikoishia muasisi wa imani yako alipo ishia ndipo na wewe utakapoishia ukifuata kwa bidii. Ila pia kwa kusoma maandiko tunaambiwa hakuna jina jingine tulilopewa la wokovu ila ni moja tu, ni Yesu Kristo pekee, utake usitake.(Matendo ya mitume 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.)
Injili ya kweli msisitizo mkubwa ni watu kuacha dhambi kumgeukia Mungu na kuokoka, kukombolewa kitu ambacho hata malaika mbinguni hushangilia (Luka mtakatifu 15:7 Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu) na hayo mengine ya mwilini tutajaliziwa. Na huo ndio msingi mkubwa ili kumsaidia mtu kumponya mwili na roho, na kumfundisha muumini ajue jinsi ya kutotegemea watu, mtu au vitu bali Mungu pekee aliye kila mahali.
Ukimfuata Mungu na kumtumikia siku ya mwisho ikifika Yesu atakaporudi lazima akuchukue siku ya unyakuo ikifika, kama Yesu alivyoahidi na kusisitiza kuwa mbingu na nchi zitapita lakini maneno yake hayatapita kamwe.
Kimbilia kwa Yesu haraka kipindi hiki una uhai, ukifa itakuwa hamna nafasi tena ya kutengeneza, tengeneza na Mungu wako sasa hujui ya kesho imepangwa nini kwako. Mithali 27:1 Usijisifu kwa ajili ya kesho; kwa maana hujui yatakayo zaliwa na siku moja.
Kila mmoja atasimama yeye peke yake na Mungu kutoa hesabu ya matendo yake alipokuwa duniani, wazazi hawatajibia watoto, wala watoto hawatawajibia wazazi (Warumi 14:12 Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.)
Enyi manabii wa uongo nawasihi acheni kuwapotosha watu wa Mungu, Mungu anawaona uganga mnaotumia na kuwahadaa na kupata pesa zina mwisho. Itakusaidia nini uwe tajiri na mali mengi fedha, magari, majumba harafu uikose mbingu? (Mathayo 16:26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?)
Hata ipigwe kelele vipi, Manabii, Watumishi, waalimu, maaskofu, mitume, wainjilisti, wachungaji wa uongo wataendelea na kuongezeka, kama maandiko matakatifu yalivyotabiri kabla.
Siku hizi kumekuwa na watumishi wengi waliojiingiza katika utumishi na kufanya kazi ya Mungu ni kama ajira mbadala na sio kazi ya wito, inafananishwa na kazi ya mshahara, wanasimamia andiko (1Wakorintho 9:14 Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo injili).Hofu ya Mungu inapotea taratibu. Asilimia kubwa ya watu wanaokosa ajira, hujiingiza kwenye utumishi wa Mungu,Uchungaji, uaskofu, unabii, ila kwa mtazamo wa maandiko, swala la kushuhudia kila mtu amjue Kristo, ni jukumu la kila muumini, biblia haikusema watumishi wote tufungue makanisa na kujipachika ma vyeo na wake zetu (Marko mt. 16:15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe) unaweza kushiriki kwa kuingia moja kwa moja au hata kuchangia huduma hizo nawe kwa namna moja au nyingine utakuwa umeshiriki na umefanya ushuhudiaji, na una thawabu yako katika huo utumishi. Pia sio lazima wote tuwe wachungaji, maaskofu, manabii, waalimu, fanya kwa upande wa kile ulichobarikwa, nacho, unaweza kusaidia kazi ya Mungu katika maeneo mbali mbali nawe ukawa una fungu lako katika huduma husika. Amua kusimama na watumishi mbali mbali wa Mungu ili kuisukuma kazi ya Mungu, Duniani hapa tunaishi kwa utofauti tofauti, kuna watu Mungu anawatumia mno lakini hawana uwezo wa kuendesha huduma zao, sababu wana changamoto ya fedha, na wengine wana fedha za kumwaga, simama katika eneo hilo hilo saidia kazi mbali mbali za Mungu ili Mungu apate utukufu pia nawashauri wamwombe Mungu awasaidie jinsi ya kuzitumia pesa kwa busara katika mapenzi yake, ili pia kupata ulinzi wa ki Mungu. Enzi za Yesu kulikuwa na watu ambao walikuwa na fedha zao mf.Yusufu Arimathaya, hakujitokeza mara kwa mara lakini Yesu alipokufa wanafunzi waliingiwa na hofu kuu, hawakuwa na ujasiri tena Mungu anamtumia Tajiri Yusufu Arimathaya (Mathayo mt 27: 57 Hata ilipokuwa jioni akafika tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;) (Sio lazima watu wote wawe miongoni mwa wanafunzi wa Yesu, lakini wanaweza kutumika sehemu fulani na thawabu yao haitawapotea Mungu ni mwaminifu)
Watu wengi wanavutiwa na huduma hizo za watumishi hao wa uongo, sababu moja inayopelekaa watu kila siku kumiminika ni miujiza na sio Yesu mtenda miujiza na baadhi ya hao manabii hutoa chakula cha mwilini mf,Mchele, soda Nyama, Sukari,etc bure na ukisha ingia kwenye huduma hizi unashindwa kuchomoka labda neema ya Mungu ikupitie uchomoke na kulijua neno la Mungu.Maandiko yapo wazi yanaposema yawezekanaje kipofu kumwongoza kipofu mwenzie je hawatatumbukia shimoni wote wawili?
(Luka Mt 6:39 Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?)
Siku hizi kuna idadi kubwa ya watu hawahudhurii kabisa nyumba za ibada sababu ya viroja vinavyotokea kwenye nyumba za ibada na kukwaza mtu mmoja mmoja, mtu anaona ni kheli akae nyumbani tu kama akifa, atazikwa tu, nyumba za ibada sio mahali tena pa kutua mizigo bali ni sehemu ya kwenda kukusanya makwazo na kuongeza stress.
Watumishi hawa waliovaa mavazi ya kondoo wanapokuwa viongozi wakuu, makanisa wameyajenga kwa jitihada na uhamasishaji wao utawaambia nini? 'kama unakwazika sepa, Makanisa si yapo mengi?'
Watumishi hao mara nyingi wanapenda kukuza majina yao kuliko majina ya Mungu, utasikia kwa kiboko ya majini na wachawi, kwa babu wa upako, kwa mfalme wa wafalme miujiza ndo kitu kikubwa kinachowavutia, sisi binadamu ni watu wa ajabu unakimbilia miujiza wakati kila dakika ipitayo Mungu anakufanyia muujiza uwezo wa kuona, kutembea, kusikia,kuhisi, kuongea, kuwaza,,kupumua, kwenda haja kubwa au ndogo, kutafuna, kumeza, kutoa jasho, kusimama, n.k kwa hiyo ni mtu wa miujiza anayetafuta muujiza na hamnaga waumini wa kudumu kwenye makanisa haya wengi ni watu wenye shida wanaotaka kuombewa, watatue shida za kimwili.
Mwisho wa siku Mungu aliye hai, hatukuzwi na Shetani anafurahia fursa hizo maana huwa anazitafuta kwa udi na uvumba (Ayubu 2:1 Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhulisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhulisha mbele za BWANA).
Pia kwenye kusanyiko la watu wa Mungu linapotokea afa mfano: Watu kukanyagana, moto, jengo kuporomoka, yaani afa lolote ambalo likapelekea watu wengi kufa, Fikiri mara mbili kwa nini afa litokee? mtumishi wa Mungu alikuwa wapi? kawaida mtumishi wa Mungu wa kweli huwa anaona mapema katika ulimwengu wa roho na ana uwezo wa kuzuia mapema kabla hayajatokea umwagikaji damu. Ukiona tukio limetokea afu ikachukuliwa bahati mbaya basi ujue, lilishapangwa hilo Amka utoke usingizini.
(Amosi 3:7 Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake)
Maana ya andiko hilo ni kuwa kwa kuwa Mungu wetu ni mkuu hakuna mwingine ila yeye peke yake ana uwezo wa kujua kila kitu kabla ya kutokea, iwe kibaya au kizuri. Kama kizuri atakujulisha na kama kibaya kuna namna fulani atakutaarifu mapema, ili uweze kuzuia kwa kutumia maombi, ili uweze kuepusha maafa na vifo. Kwa kuingia rohoni mapema na kupambana hadi ushindi upatikane, kwa kuwa Mungu ni mkuu, ushindi lazima utokee upande wa Mungu, na mtumishi wake mwisho wa siku Mungu apate utukufu, lakini ukiona tofauti, asomaye na afahamu. Sio hivyo tu ukisoma Ezekiel 18:32 Inasema (Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.) Sasa huyu anaye hua bira huruma, taarifa au tahadhari mapema ni Mungu au mungu? jibu wewe, Shetani kazi yake kuu ni kuua, kuharibu tangu mwanzo, hata kama atakufaidisha kuna mahali amekutegea, kama jogoo la Krismass unalipa chakula unajua siku yake utalichinja tu.
Ushuhuda/ushahidi
Kwa sisi tunaokaa Dar tunayaona mengi kuna mtumishi yupo anagawa upako wa kinabii anatoa mpaka number yake ya simu kwa gharama kidogo, ukishatoa pesa (sadaka) anakupa uwezo wa kumuwekea mtu mkono, kumnyoshea mkono muumini mkono anadondoka chini, ili uonekane una nguvu za ki Mungu sana, hicho mara nyingi kinawavutia watu na kuamini kuwa mtumishi husika ana tumiwa na Mungu.Ukiwa nabii una uwezo wa kumvuvia mtu umtakaye au watu uwatakao ili wakafanye miujiza ile ile inayofanywa na wewe kiroho upande giza inawezekana na kiroho upande wa nuru inawezekana, hamkumbuki kipindi kile Yesu alivyowatuma wale wanafunzi wake sabini na matokeo yaliyotokea? (Luk 10:17 Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako). pamoja na kuwa wote wanaomwamini Kristo wamepewa uwezo huo lakini pia kuna uwezekano wa kupoke special package. Kuna mawakala wa kishetani wanafuatilia baadhi ya watumishi wa Mungu ambao wanasumbua sana ufalme wao wakitaka waingie maagano nao ili wafanye kazi pamoja kwa ahadi ya kupewa msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo fedha lukuki, ili uwe maarufu fasta. Kuna baadhi ya watumishi walikuwa moto lakini sasa wamekuwa baridi, kuna baadhi ya hawa watumishi wametangulia mbele ya haki na wengine wapo hai bado, nahisi Mungu anawapa neema ya uhai ili wageuke na kutubu ila wasipoifanyia kazi nadhani Mungu anaweza kughairi.
Makanisa na yaendelee kuzuka tu maana imeshatabiliwa ila ole wao wasiomwamini Kristo na kuona kuwa Yesu hakufanya chochote kajipendekeza tu kutufia Msarabani, itawagharimu.Kitu kizuri kingine ni kuwa ukiwa na Roho Mtakatifu ukiingia kwenye blog, Youtube,facebook au kuingia kwenye kanisa linaloongozwa na nabii au mtumishi asiye wa Mungu utapata signal tu na kujua kuwa huyu ni wa Mungu au mungu anayetawala madhabahu husika.
Ukifuatilia kwa undani watu wengi wanaofurika kwa Manabii, mitume, wa uongo na kutapeliwa ni Wakristo au waumini wa dini nyingine ambao hawana neno la Mungu (Biblia ) ndani ya mioyo yao na kuliishi.Pia ni wavivu wa kusoma na kufuatilia neno la Mungu aliye hai, Mtu unayelijua neno la Mungu huwezi kutapeliwa kizembe zembe na kuangukia kwenye majuto ambayo yanaweza kupelekea kuamini watumishi au Manabii wote ni matapeli wakati wapo wengi wazuri wanatabiri yanatokea na Mungu anatukuzwa.
Baadhi ya makanisa uwepo wake ni msukumo wa mtu au watu furani matajiri wenye pesa zao basi kanisa linazuka, kuna kanisa moja lipo Mbeya lenyewe linaruhusu wake wengi na kunywa pombe nyingi ni sehemu ya ibada na lina waumini, siku nikipata jina lake nitakuja kulitaja hapa hapa.
Kawaida sisi kama binadamu kawaida ukitendwa mabaya, mfano umetapeliwa, umebakwa, umeumizwa utakuwa na chuki na watu wote waojiita Watumishi wa Mungu (kwa kutojua kupambanua kati ya watumishi wa Mungu muumbaji na watumishi wa mungu wa dunia hii) kitendo cha kuwachukia, kuwanenea maneno magumu, watu wanaojiita watumishi, ukiwachukia watumishi wa Mungu wa kweli unaweza kuingia katika mgogoro mwingine na Mungu aliye hai. (Mwanzo 27:29 Mataifa na wakutumikie na Makabila wakusujudie,Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako wakusujudie. Atakayekulaani alaaninwe, Na atakeyekubariki abarikiwe). ( Kwa imani sisi sote ni wana wa Ibrahimu). Kwenye biblia kuna kipindi Musa alioa mwanamke Mkushi, Harusni na Miriam wakamta Musa kwa kitendo chake cha kumuoa mwanamke Mweusi, kitendo hicho kilipelekea Miriam Kupata pigo kutoka kwa Mungu (Hesabu 12:1 - 15 Kisha Miriam na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya Mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana; alikuwa amemwoa Mwanamke Mkushi. Wakasema, Je ! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu ? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao. ... Sio hivyo tu unaweza ukawa na hasira na hata ya kuhudhulia ibada, ukaona ni mambo ya hovyo tu, usanii mtupu hata huyo Mungu mwenyewe sijui hata kama yupo si angezuia lisikutokee? Usiposhiriki ibada unavunja amri ya Mungu ya nne. Ukimkosea Mungu unakuwa umemfungulia, umemrahisishia Shetani kazi kukupiga vizuri. Ni kama vile mamba ili akushambulie vizuri uingie kwenye 18 zake uwe kwenye maji, sio nchi kavu.
Naomba niishie hapo lakini nataka ujue kuwa Shetani hajalala, halali akitutafuta ili tupotee na kwenda kwenye mauti ya milele pamoja naye, Mpendwa mkimbilie Yesu usije ukaingia kwenye moto wa milele aliowekewa Shetani na malaika zake walioasi.MKIMBILIE YESU LEO, USISUBIRI KESHO.
" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.
Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.
1. Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
2. Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
3. Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
(Waebrania 10:25).
6. Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
Ni mimi
Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
injiliyajioni@gmail.com
www.injilijioni.blogsport.com