Maana
ya ibada ni tendo la heshima ya hali ya juu linalotolewa kwa mwenyezi Mungu au
kwa chochote kile kinachoheshimiwa kama Mungu, inaweza kufanywa na mtu binafsi
au kundi hasa likiongozwa na kuhani au mwingine anayekubalika. Ibada
inajumuisha vitendo kama vile kuomba, kusifu, kuabudu, kusujudu, kuimba,
kufunga , kutoa sadaka na kushiriki maagano mbali mbali.
Kuna aina ngapi za ibada?
Ibada zipo za aina nyingi hakuna
idadi kamili za ibada ila kila mtu anatakiwa afanye kile anachotakiwa
kufanya mradi tu havunji sheria za nchi husika, ibada inatakiwa kufanyika
kwa hiyari ya mtu binafsi na sio kwa kushurutishwa. Pia kila mmoja anatakiwa
aheshimu imani au ibada ya mtu mwingine. Katika dunia hii tuliyopo kuna watu
wanaabudu Mungu na wengine na wengine wanamwabudu shetani, wengine wanaabudu
vitu, mfano jua, mwezi, wanyama wakubwa, wanyama wakali, milima mirefu,
majabari na wengine wanaabudu timu za mipira, vyama vya siasa, movie za tv n.k.
Na hivi dunia inavyoelekea ukingoni si ajabu zikaibuka imani ngeni nyingi za
ovyo kama maandiko matakatifu yalivyotabiri kabla.
Kusudi la kuumbwa kwetu
Mungu alituumba ili tumwabudu yeye
peke yake na sio kingine chochote na ndio amri yake kuu ya kwanza kumwabudu yeye
na kutoabudu kitu kingine chochote kisicho Mungu, Shetani naye anatamani
aabudiwe yeye peke yake. Ibada isiyo mpendeza Mungu itampendeza Shetani na
baadhi ya matunda yake kuanza kuonekana, baadhi ya matunda ya shetani (Wagalatia 5:19-21 Basi matendo ya mwili ni dhahiri,
ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi,
wivu, hasira, fitina, faraka,uzushi, husuda, ulevu, ulafi …Na Mungu mtakatifu akiabudiwa uwepo wake
utajidhihirisha na baadhi ya matunda yake huweza kutokea (Wagalatia 5:22-23 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha,
Amani, uvumilivu, utu wema, fadhili,
uaminifu, upole, kiasi …)
(Mathayo Mt 22:35-38 Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza ,
akamjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? akamwambia, mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa akiri zako zote.Hii
ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza) Mungu huyu pia ni Mungu mwenye
wivu kwa hiyo kukipa nafasi kubwa, heshima, mapenzi , muda, fedha, nguvu kitu
kingine chochote zaidi ya Mungu ni kukiabudu kitu husika hii ni hatari sana
inaweza kukuletea mgogoro na Mungu Mtakatifu, hatutakiwi kushindana na Mungu
sisi ni binadamu tu ni mavumbi tu.(Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na
mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka
mia na ishirini (Mwanzo 6:3 BWANA
akasema, Roho yangu haitashindana na milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama;
basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.) Ingawa Mungu yeye ndio
mwumbaji lakini bado anatushauri , hatulazimishi anatuelekeza kwa upole
kumwabudu yeye peke yake. Uamuzi wa upande gani muumini kuchagua ni hiyari yake
mwenyewe kama kwa Shetani au Mungu huyu Mtakatifu. Mtume Paulo mahari fulani
amewahi kutoa ushauri (1Kor 10:14 Kwa
ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.) Ila pia tujue
ya kuwa Shetani hana mpango mzuri na binadamu yoyote anayeishi duniani sasa.
Kuna baadhi ya watu wapo hapa duniani wanapewa na wanapata utajiri kupitia
kutoa makafara ya damu kuua watu wanao wauwa ili kutajirika ole wao wafanyao
haya mambo maana yote wanayoyafanya hata wakifanya kwa Siri gizani Mungu
anayaona kama mchana kweupee. Na pia kwa kuwa vitu vyote ni watumishi wa Mungu,
(Zaburi 119:91 Kwa hukumu zako vimesimama imara
hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.) Mungu anaweza kutumia chochote kikampa taarifa.
Itakusaidia nini ndugu yangu upate mali zote za dunia harafu uikose mbingu? (Marko
8:36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya
nafsi yake?
Kwa ushauri kuhusiana na ibada ni
vizuri na inapendeza kuchagua eneo maalumu kwa ajili ya kufanyia ibada sio kila
mahari panafaa. Dunia ina siri nyingi hasa kwenye mchanga, ardhi. Ni vizuri
kulitakasa eneo fulani kwa ajili ya ibada na hapo ndo pawe mahali pako pa
kufanyia ibada, hata kama ni nyumbani pako unapoishi sio kila siku kubadilisha
eneo changua eneo fulani kwa ajili ya kuabudia sio mara leo hapa kesho kulee
sio hivyo. Tujifunze kwa kwa baba yetu wa Imani Ibrahimu kama alivyoelekezwa na
Mungu aende akatoe sadaka kule kwenye nchi ya Moria, pamoja na kuwa zamani
idadi ya watu ilikuwa ndogo kwa hiyo maeneo mengi yalikuwa wazi (Mwanzo 22:2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana
wako wa pekee, umpendaye, Isaka ukaende zako mpaka Nchi ya Moria, ukamtoe
sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia) ndio maana karibu dini zote hata za kisheani na
wachawi wanakuwaga na maeneo maalum ya kufanyia ibada mfano kwenye pango fulani
au kwenye mti wa Mbuyu.
Na jambo jingine la kulitambua ni
kuwa Mungu ni Mtakatifu mno basi kabla ya kumwabudu ni lazima kuwa safi mwili na roho na kila kitu ulicho nacho
uweke pembeni Cheo, kazi , heshima, utajiri, nguvu na kufanya toba ya kweli
ukimaanisha (Yohana mt 4:24 Mungu
ni Roho nao wammwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na kweli
pia sehemu nyingine inajieleza kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi (Yohana mt 9:31 Twajua ya kuwa Mungu
hawasikilizi wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi
yake, humsikia huyo)
Ukimwabudu Mungu automatic
utampenda, "kama unampenda mtu au mpenzi wako utatamani kila siku
umpendeze, ufanye vile apendavyo" kwa habari ya Mungu muumbaji wa mbingu
na nchi usingetamani kumkosea, kuvunja naye mahusiano, kumkorofisha na
utajitahidi upendo wenu baina yenu nyie wawili udumu na kukua. Na kwa vyovyote
vile ukijitahidi kuwa karibu naye atakuonekania tu, maana ameahidi kuwa ( Nanyi
mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote (Yeremia 29:13 pia mtafuteni Bwana,
maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu) (Isaya 55:6 Mungu si mtu, aseme uongo; Wala
si mwadamu ajute; Iwapo amenena, hatafikiliza? ila pia ukimtafuta Mungu
utakuwa na uvuvio wa kiungu na ukimtafuta Shetani utakuwa na uvuvio wa kipepo.
Mungu wa Israel, aliyetupa mimi na
wewe pumzi ya uhai, huyu aliyeziumba mbingu na nchi Yehova Mungu aliyeketi juu
sana lakini pia kwa uwezo wake usio weza kuelezeka yupo karibu nasi mno mno kwa
jinsi ya ajabu, Mungu ambaye hawezi kuelezeka kwa jinsi alivyo, nguvu zake,
upendo wake, uwezo wake, fadhili zake, ulinzi wake, neema zake, siri zake, n.k
Tunapokwenda mbele za Mungu ni
lazima tuende kwa heshima na adabu mno, kama mashetani na mapepo wanatetemeka
wanapolitaja jina lake Mungu sisi binadamu ni nani hata tulete dharau?
Tabia mbaya zinazofanywa na baadhi ya waumini wasio heshimu
ibada
- Kutozima zima simu au kuongea
ongea kusikokuwa na uhusiano na ibada huku ibada ikiendelea.
- Kuwasha redio/mziki kwa sauti
ya juu wakati ibada ikiwa imeanza au inaendelea ( hii inawahusu wale wote
waliojenga nyumba zao karibu na nyumba za ibada)
- Baadhi ya waumini huvaa nguo
chafu, zinazonuka, mavazi yanayovaliwa kwenye majumba ya starehe hupelekea
kukwaza wengine waliokuja kumwabudu Mungu serious. Ole wake anayeleta
makwazo kwa wengine (Luka mt 17:1
Akawaambia
wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye
yaja kwa sababu yake !.
- Kuna baadhi ya nyumba za ibada
zina majengo makubwa mazuuri mno lakini wafadhiri wake wakuu wa majengo
haya ni watu waliopata fedha haramu mfano ualifu, usagaji, ushoga, uuaji
kiongozi ukijua chanzo kama kibaya usichukue fedha hizo italeta dosari,
kama hujui sawa.
- Baadhi ya waumini au wahudumu
wa ibada wana matendo maovu kama niliyoyataja hapo juu halafu wanakuja
kuongoza au kushiriki ibada ni mbaya huko ni kujitafutia laana, Mungu
hadhihakiwi. Unatakiwa uchague upande mmoja kwa Shetani au kwa Mungu sio
kwa Mungu unakutaka na kwa Shetani unakutaka. Usiwe vugu vugu chagua kuwa
moto au kuwa baridi. (Ufunuo 3:15
Nayajua
matendo yako, ya kuwa hu baridi wala moto; ingekuwa heri kama ungekuwa
baridi au moto)
- Nyumba za ibada zinatakiwa ziwe
na utulivu wa hali ya juu sio vurugu vurugu mfano wamachinga, dala dala na
wapiga debe. Kama itatokea changamoto kama hiyo na haiwezekani kuhamisha
jengo basi waumini wapambane waweke viyoyozi ili kusiwe na muingiano wa
sauti za nje na sauti za ndani. Hata Yesu hapendi makelele yasiyohusiana
na ibada (Mathayo mt 21:12-13 Yesu akaingia ndani ya
heakalu, akawafuza wote waliokuwa
wakiuza na kununua hekaluni, akapindua meza za wabadili fedha, na viti
vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi)
- Kuna wachungaji, manabii
wanakufuru kwa kupayuka payuka Madhabahuni, zamani ilikuwa mtu anayeenda
madhabahuni patakatifu pa patakatifu alikuwa anafungwa kamba mguuni ili
kama atakuwa ameuawa kwa kukiuka atolewe nje. Siku hizi neema iliyopo
inatuzubaisha mpaka heshima
imepungua, kuna watu wanaongea ya uongo madhabahuni kuna Nabii mmoja amejigamba hivi karibuni kuwa Yesu
atakaporudi atapanda gari lake jipya atamchukua toka kiwanja cha ndege na
kwenda katika ibada kanisani kwake hii haiko sawa. kuwaombea mabaya
viongozi fulani fulani ili either wafe, wapate ajari hiyo si kazi ya
ukristo kazi yetu kuwatakia na kuwaombea amani wote wabaya kwa wazuri.
- Kuthamini mambo mengine ya
kidunia na kuyapa kipaumbele kuliko ibada ni kosa baadhi ya mambo kama
vile Mapenzi, starehe, kazi na majukumu yetu ya kila siku
Mungu ni Mungu wa walio hai wenye
uwezo wa kufanya ibada, Mungu si Mungu wa wafu kwa maana hiyo basi ni vizuri kutengeneza
mahusiano mazuri na Mungu wakati ukiwa bado hai, siku tutakapo kuwa tupo
jenezani au kaburini tutakuwa hatuna sifa tena ya kuwasilana na Mungu safari
itakuwa imeishia hapo. Haijalishi kama watu watakao kuwa hai watamsihi Mungu
akupunguzie adhabu au akusamehe. Hakuna mtu yeyote duniani wa kuweza kumgeuza
Mungu mawazo yake analotaka ndo huwa au hutokea. Haijalishi ni Maaskofu, mashehe, Mapadre, maimamu, hata kiwe
cheo gani ili mradi ni mwanadamu Mungu ni Mungu na mwandamu ni mwanadamu tu, na
udongoni tutarudi tutake tusitake ndo Mungu alivyokwisha sema katika maandiko
yake. (Mwanzo 3:19 Kwa
jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo
ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi)
Kuna tabia imeenea miongoni mwa
baadhi ya watumishi wa Mungu wasiomjua Mungu aliye hai ya kugoma kwenda
kushiriki baadhi ya ibada za mazishi hasa iwapo itajulikana kama marehemu
alikufa vibaya kwa kukamatwa ugoni, kunyongwa, au kujinyonga, kunywa sumu,
kumeza vidonge au kujiua kwa makusudi kwa namna yeyote ile. Lengo la kuu la
kwenda kufanya ibada kwenye mazishi yeyote ni kupeleka injili ya Yesu Kristo
kwa watu wote, kuna watu hawahudhulii ibada za kwenye nyumba za ibada kabisa
lakini nafasi kama hizi ni fursa ya pekee ya kwenda kulitangaza jina la Yesu
Kristo kwa kila kiumbe. Maandiko matakatifu yanatusisitiza kupeleka injili kwa
kila kiumbe aamniye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa. (Marko mt 16:15-16 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni
mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka;
asiyeamini, atahukumiwa)
Kugoma, kutokwenda kufanya ibada ni
kuhukumu huko, kama wakristo hatutakiwi kuhukumu hilo ni jukumu la Mungu
mwenyewe (Mathayo mt 7:1 Msihukumu,
msije mkahukumiwa ninyi) Kama Yesu mwana wa Mungu aliye hai, aliwahi
kuletewa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi na mashuhuda watu wazima
walioshuhudia tukio lenyewe hakumuhukumu, wewe ni nani hata ufanye hukumu? Huna
uovu wewe? (Yohana mt 8:3 – 11 Waandishi
na Mafarisayao wakamleta mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati…
Vile vile Mungu huyu huyu Mtakatifu
hapendi yeyote apotee bali wote waifikie toba. (2Petro 3:9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama
wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana
hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba). Vile vile Mungu
hakufurahii kifo chake mwenye dhambi (Ezekieli
33:11-12 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kufa
kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya
akaishi.Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa,Enyi
nyumba ya Israeli?)
Ukizingatia hizi ni siku za mwisho zilizotabiriwa ni lazima injili ihubiriwe kwa
kila njia iliyopo na kwa gharama yeyote ile, ili kukamilisha kusudi la Mungu
alilolikusudia, siku hizi kuna njia, vyombo vingi ambavyo kwavyo injili ipitie
Youtube, Whatsapp, Twitter, snap chart, Tick Talk, google, Face book,
Instagram, Telegram, WeChat na Pinterest na nyingine nyingi, vyote hivyo ni
vibebeo vya injili ya Kristo tunapaswa kuvitumia, maana maeneo yote hao kuna
viumbe. Mungu wetu ni tajiri vyote ni mali yake dunia na wote wakaao ndani
yake.
BAADHI YA FAIDA/MANUFAA YA KUFANYA IBADA AMBAYO NI KUMCHA BWANA
1. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunaongeza siku za kuishi (Mithali 10:27 “Kumcha Bwana kwaongeza siku za
mtu; Bali miaka yao wasiohaki itapunguzwa”)
2. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunafungua mlango wa maarifa (Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha
maarifa
, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.) (Danieli 1:17-20 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu
aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na
ufahamu katika maono yote, na ndoto. Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme
za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza, mbele ya mfalme Nebukadreza. Naye
mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama
Danieli, na Hanania na Mishaeli na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.)
3. Kufanya ibada, kumcha Bwana kuna imarisha umoja wetu na
Mungu, kwa kawaida mwanadamu anapokuwa mbali na Mungu anakuwa mpweke, na
mnyonge na kukosa furaha ya kweli.Siku za nyuma katika nchi yetu swala la ibada
lilipewa kipaumbele sana, ilikuwa kila shule inajipangia siku mojawapo katika
wiki inaweza kuwa Jumatano au ijumaa kila mtoto ataenda kwenye dhehebu lake
analoabudu japo kwa masaa kadhaa, siku hizi yamepungua sana au hayapo kabisa
kwa baadhi ya shule kama shule itakuwa sio ya kimishenary. Mkazo uliopo sasa
hivi ni watoto kufaulu kwa kiwango cha A. Binafsi mimi nimekulia katika ibada
za shuleni tangu udogo. Ukimpa mtoto malezi ya dini sio rahisi ayaache
atakapokuwa mtu mzima (Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee)
kila mtu ana uhitaji wa kufanya ibada hata wafungwa waliopo gerezani wanatakiwa
wapatiwa nafasi ya kufanya ibada kulingana na imani yake, hilo ni hitaji kuu la
moyo wa mwanadamu yeyote mwenye pumzi ya uhai.
4. Kufanya ibada, Kumcha Mungu kutakupelekea kupata uzima wa
milele (Mithali 14:27 “Kumcha
Bwana ni chemchemi ya uzima, ili kuepukana na tanzi za mauti”)
5. Kufanya ibada, kumcha Mungu unapata hekima (Zaburi 111: 10 Kumcha Bwana ndio mwanzo wa
hekima wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa zake zakaa milele.
6. Kufanya ibada, kumcha Bwana ni ulinzi kwako na watoto wako
(Mithali 14:26 Kumcha Bwana ni tumaini imara;
watoto wake watakuwa na kimbilio.)
7. Kufanya ibada, kumcha Bwana ni utajiri (Mithali 22:4 Thawabu ya unyenyekevu ambao ni
kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.)
8. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunatupa nguvu ya kuangusha
ngome na vifungo vya adui (Marko mt 9:28-29 Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake
wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? . Akawaambia, Namna hii
haiwezi kutoka kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.)
9. Anayependa ibada hata akipata changamoto yeyote hawezi toka nje
mstari akamkosea Mungu Mfano Ayubu, Abrahamu na mkewe na changamoto ya kutopata
mtoto mapema, Danieli na wenzake. Kuna vita katika maisha yako hautaweza
kushindana nayo mpaka utakapoamua kuwa mtu wa ibada.
10. Kufanya
ibada kunaleta majibu ya maswali ya maswali mbali mbali yanayotutatiza Roho
Mtakatifu msaidizi wetu mkuu hawezi kutuaacha katika kila hali tunayopitia,
mitego yote ya siri huteguliwa hata katika ulimwengu wa roho, hakuna jambo
jambo gumu la kumshinda Mungu.
Kiuhalisia
haitakiwi kuegemea kwenye siku moja katika wiki bali kila siku ni siku ya
kumfanyia Mungu wetu ibada, Ni kosa sana kuegemea katika siku sahihi ya kweli
kufanya ni Jumamosi au Jumapili tu, Mungu anatakiwa kufanyiwa ibada kila siku
iitwayo leo. Kwa sababu rehema zake kila siku ni mpya basi basi na tumsifu,
tumshukuru, tumwombe, tumwabudu, tumfanyie ibada, tumpende, tumwimbie, tumtolee
sadaka kila siku.
Sio
kila mtu anafaa kuongoza ibada, sio kila mtu ni mtumishi wa madhabahuni kumtumikia
Mungu sio lazima kusoma elimu ya juu sana kama PHD na kadhalika ni wale
waliokubaliwa na Mungu mwenyewe na mtu wa kuongoza huwa anakuwa na kibari
kutoka kwa Mungu ukimwona tu huulizi sio kazi kama ya watu wa duniani. Kwa kuwa
ibada ni ya Mungu mtakatifu mwenyewe kwa hiyo hata waongozaji Mungu hujitafutia
mwenyewe kwa kuomba uongozi wake na msaada kutoka kwa Roho Mtakatifu wake. Wote
wanaolazimisha kawaida wataona huduma ni ngumu sana, maana watatumia akiri na
usomi wao, usipate msukumo wa kufanya ibada sababu ya changamoto fulani
inayokusibu maishani baadhi ya changamoto ni kukosa kazi, kustaafu na uchumi
kuyumba, ugonjwa mkubwa usioponyeka kirahisi, kukosa mchumba nk, bali ibada
inatakiwa iwe ni sehemu ya utaratibu wako wa maisha.
Pia ni
kosa kufanya ibada za wafu, hiyo ni kufanya ibada za mizimu, kukaribisha
mashetani katika maisha yako shetani hana urafiki na mtu yeyote, unaweza sema
mbona baadhi ya watu wanafanikiwa kwa nguvu nyingine? Hawa watu utajiri
waupatao una masharti magumu kiasi ambacho hupelekea kujutia maishani na moto
wa jehanamu wa milele unawasubiri baada ya maisha haya mafupi ya hapa duniani.
Shetani hafanyi kitu kwa hasara. Ni kama kuku anayelishwa vizuri amewekwa tayari
kwa ajiri ya sikukuu inayokuja. Hapa pia kuna watu wanajiita watumishi wa Mungu
lakini wanatumia nguvu nyingine ole wao, Mungu aonaye sirini anawaona kweupee.
Wanawapotosha watu wasimjue Mungu wa kweli pia wamchukie Mungu.
Asili
ya ibada na vitu vyote vinavyoambatana na ibada ni Mungu mwenyewe. Vitu
vinavyoambatana navyo ni Sadaka na Ngoma
SADAKA
Aliyetoa
sadaka njema na ya thamani kuliko wote ni Mungu Mtakatifu mwenyewe, na sadaka
inatofautiana uzito, aliyetoa sadaka ya kuku au njiwa si sawa na aliyetoa
sadaka ya ngombe.
(Yohana mt 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.) Hata katika
Kitabu cha Mwanzo walipoumbwa Adamu na Hawa Mungu alitoa sadaka. (Mwanzo 3:21 BWANA Mungu akawafanyia Adamu na
mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Pia kuna baadhi ya watu waliwahi
kufanya mdhaha na kipengele hiki cha ibada (Matendo yaMitume 5:1-11 Anania
na Safira Mungu alivyowaadhibu hadharani.
NYIMBO/SIFA/NGOMA
Asili
ya ngoma, nyimbo, sifa ni mbinguni malaika wanamuimbia Mungu usiku na mchana
bila kuchoka, kuna muimbaji mmoja aliwahi kuuliza swali “mziki asili yake wapi?”
Mziki asili yake ni mbinguni.
Habari
za mbinguni nyingi zimefichwa ingawa kitabu cha ufunuo kwa sehemu kimetudokezea
kidogo (Ufunuo wa Yohana 4:8 Na hawa wenye uhai wanne, kila
mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala
hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana
Mungu mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.
Mziki
na dansi tulizo nazo leo duniani shetani amekopi na ku paste kutoka kwa Mungu Mtakatifu
yeye si unajua alikuwa karibu na Mungu mno. (Ezekiel 28:14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta
afunikaye; name nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu,
umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.
Kati ya huduma tuzifanyazo hapa duniani ambayo itakuwa na muendelezo mpaka mbinguni ni uimbaji wa kumsifu Mungu wetu.Tutamsifu bila kuchoka tukiwa na miili mipya ya mbinguni. Naamini utakuwa umejifunza kitu, asante kwa kuchukua muda kujifunza ujumbe wa neno la Mungu endelea kujifunza kupitia masomo mengine
" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.
Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.
1. Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
2. Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
3. Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
(Waebrania 10:25).
6. Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
No comments:
Post a Comment