Thursday, September 5, 2024

USIFANYE UTANI NA IBADA



Maana ya ibada ni tendo la heshima ya hali ya juu linalotolewa kwa mwenyezi Mungu au kwa chochote kile kinachoheshimiwa kama Mungu, inaweza kufanywa na mtu binafsi au kundi hasa likiongozwa na kuhani au mwingine anayekubalika. Ibada inajumuisha vitendo kama vile kuomba, kusifu, kuabudu, kusujudu, kuimba, kufunga , kutoa sadaka na kushiriki maagano mbali mbali.

Kuna aina ngapi za ibada?

Ibada zipo za aina nyingi hakuna idadi kamili za ibada  ila kila mtu anatakiwa afanye kile anachotakiwa kufanya mradi tu havunji sheria za nchi husika, ibada inatakiwa kufanyika  kwa hiyari ya mtu binafsi na sio kwa kushurutishwa. Pia kila mmoja anatakiwa aheshimu imani au ibada ya mtu mwingine. Katika dunia hii tuliyopo kuna watu wanaabudu Mungu na wengine na wengine wanamwabudu shetani, wengine wanaabudu vitu, mfano jua, mwezi, wanyama wakubwa, wanyama wakali, milima mirefu, majabari na wengine wanaabudu timu za mipira, vyama vya siasa, movie za tv n.k. Na hivi dunia inavyoelekea ukingoni si ajabu zikaibuka imani ngeni nyingi za ovyo kama maandiko matakatifu yalivyotabiri kabla.

 

Kusudi la kuumbwa kwetu

Mungu alituumba ili tumwabudu yeye peke yake na sio kingine chochote na ndio amri yake kuu ya kwanza kumwabudu yeye na kutoabudu kitu kingine chochote kisicho Mungu, Shetani naye anatamani aabudiwe yeye peke yake. Ibada isiyo mpendeza Mungu itampendeza Shetani na baadhi ya matunda yake kuanza kuonekana, baadhi ya matunda ya shetani (Wagalatia 5:19-21 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka,uzushi, husuda, ulevu, ulafi  …Na Mungu mtakatifu akiabudiwa uwepo wake utajidhihirisha na baadhi ya matunda yake huweza kutokea (Wagalatia 5:22-23 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, Amani, uvumilivu, utu wema, fadhili,  uaminifu, upole, kiasi …) 

(Mathayo Mt 22:35-38 Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza , akamjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? akamwambia, mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa akiri zako zote.Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza) Mungu huyu pia ni Mungu mwenye wivu kwa hiyo kukipa nafasi kubwa, heshima, mapenzi , muda, fedha, nguvu kitu kingine chochote zaidi ya Mungu ni kukiabudu kitu husika hii ni hatari sana inaweza kukuletea mgogoro na Mungu Mtakatifu, hatutakiwi kushindana na Mungu sisi ni binadamu tu ni mavumbi tu.(Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini  (Mwanzo 6:3 BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.) Ingawa Mungu yeye ndio mwumbaji lakini bado anatushauri , hatulazimishi anatuelekeza kwa upole kumwabudu yeye peke yake. Uamuzi wa upande gani muumini kuchagua ni hiyari yake mwenyewe kama kwa Shetani au Mungu huyu Mtakatifu. Mtume Paulo mahari fulani amewahi kutoa ushauri (1Kor 10:14 Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.) Ila pia tujue ya kuwa Shetani hana mpango mzuri na binadamu yoyote anayeishi duniani sasa. Kuna baadhi ya watu wapo hapa duniani wanapewa na wanapata utajiri kupitia kutoa makafara ya damu kuua watu wanao wauwa ili kutajirika ole wao wafanyao haya mambo maana yote wanayoyafanya  hata wakifanya kwa Siri gizani Mungu anayaona kama mchana kweupee. Na pia kwa kuwa vitu vyote ni watumishi wa Mungu, (Zaburi 119:91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.)  Mungu anaweza kutumia chochote kikampa taarifa. Itakusaidia nini ndugu yangu upate mali zote za dunia harafu uikose mbingu? (Marko 8:36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

 

Kwa ushauri kuhusiana na ibada ni vizuri na inapendeza kuchagua eneo maalumu kwa ajili ya kufanyia ibada sio kila mahari panafaa. Dunia ina siri nyingi hasa kwenye mchanga, ardhi. Ni vizuri kulitakasa eneo fulani kwa ajili ya ibada na hapo ndo pawe mahali pako pa kufanyia ibada, hata kama ni nyumbani pako unapoishi sio kila siku kubadilisha eneo changua eneo fulani kwa ajili ya kuabudia sio mara leo hapa kesho kulee sio hivyo. Tujifunze kwa kwa baba yetu wa Imani Ibrahimu kama alivyoelekezwa na Mungu aende akatoe sadaka kule kwenye nchi ya Moria, pamoja na kuwa zamani idadi ya watu ilikuwa ndogo kwa hiyo maeneo mengi yalikuwa wazi (Mwanzo 22:2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka ukaende zako mpaka Nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia) ndio maana karibu dini zote hata za kisheani na wachawi wanakuwaga na maeneo maalum ya kufanyia ibada mfano kwenye pango fulani au kwenye mti wa Mbuyu.

 

Na jambo jingine la kulitambua ni kuwa Mungu ni Mtakatifu mno basi kabla ya kumwabudu ni lazima  kuwa safi mwili na roho na kila kitu ulicho nacho uweke pembeni Cheo, kazi , heshima, utajiri, nguvu na kufanya toba ya kweli ukimaanisha (Yohana mt 4:24 Mungu ni Roho nao wammwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na kweli pia sehemu nyingine inajieleza kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi (Yohana mt 9:31 Twajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo) 

 

 

Ukimwabudu Mungu automatic utampenda, "kama unampenda mtu au mpenzi wako utatamani kila siku umpendeze, ufanye vile apendavyo" kwa habari ya Mungu muumbaji wa mbingu na nchi usingetamani kumkosea, kuvunja naye mahusiano, kumkorofisha na utajitahidi upendo wenu baina yenu nyie wawili udumu na kukua. Na kwa vyovyote vile ukijitahidi kuwa karibu naye atakuonekania tu, maana ameahidi kuwa ( Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote (Yeremia 29:13 pia mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu) (Isaya 55:6 Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwadamu ajute; Iwapo amenena, hatafikiliza? ila pia ukimtafuta Mungu utakuwa na uvuvio wa kiungu na ukimtafuta Shetani utakuwa na uvuvio wa kipepo.

 

Mungu wa Israel, aliyetupa mimi na wewe pumzi ya uhai, huyu aliyeziumba mbingu na nchi Yehova Mungu aliyeketi juu sana lakini pia kwa uwezo wake usio weza kuelezeka yupo karibu nasi mno mno kwa jinsi ya ajabu, Mungu ambaye hawezi kuelezeka kwa jinsi alivyo, nguvu zake, upendo wake, uwezo wake, fadhili zake, ulinzi wake, neema zake, siri zake, n.k

 

Tunapokwenda mbele za Mungu ni lazima tuende kwa heshima na adabu mno, kama mashetani na mapepo wanatetemeka wanapolitaja jina lake Mungu sisi binadamu ni nani hata tulete dharau?

 

Tabia mbaya zinazofanywa na baadhi ya waumini wasio heshimu ibada

  • Kutozima zima simu au kuongea ongea kusikokuwa na uhusiano na ibada huku ibada ikiendelea.
  • Kuwasha redio/mziki kwa sauti ya juu wakati ibada ikiwa imeanza au inaendelea ( hii inawahusu wale wote waliojenga nyumba zao karibu na nyumba za ibada) 
  • Baadhi ya waumini huvaa nguo chafu, zinazonuka, mavazi yanayovaliwa kwenye majumba ya starehe hupelekea kukwaza wengine waliokuja kumwabudu Mungu serious. Ole wake anayeleta makwazo kwa wengine (Luka mt 17:1 Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake !.
  • Kuna baadhi ya nyumba za ibada zina majengo makubwa mazuuri mno lakini wafadhiri wake wakuu wa majengo haya ni watu waliopata fedha haramu mfano ualifu, usagaji, ushoga, uuaji kiongozi ukijua chanzo kama kibaya usichukue fedha hizo italeta dosari, kama hujui sawa.
  • Baadhi ya waumini au wahudumu wa ibada wana matendo maovu kama niliyoyataja hapo juu halafu wanakuja kuongoza au kushiriki ibada ni mbaya huko ni kujitafutia laana, Mungu hadhihakiwi. Unatakiwa uchague upande mmoja kwa Shetani au kwa Mungu sio kwa Mungu unakutaka na kwa Shetani unakutaka. Usiwe vugu vugu chagua kuwa moto au kuwa baridi. (Ufunuo 3:15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto)
  • Nyumba za ibada zinatakiwa ziwe na utulivu wa hali ya juu sio vurugu vurugu mfano wamachinga, dala dala na wapiga debe. Kama itatokea changamoto kama hiyo na haiwezekani kuhamisha jengo basi waumini wapambane waweke viyoyozi ili kusiwe na muingiano wa sauti za nje na sauti za ndani. Hata Yesu hapendi makelele yasiyohusiana na ibada (Mathayo mt 21:12-13 Yesu akaingia ndani  ya heakalu, akawafuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akapindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi)
  • Kuna wachungaji, manabii wanakufuru kwa kupayuka payuka Madhabahuni, zamani ilikuwa mtu anayeenda madhabahuni patakatifu pa patakatifu alikuwa anafungwa kamba mguuni ili kama atakuwa ameuawa kwa kukiuka atolewe nje. Siku hizi neema iliyopo inatuzubaisha  mpaka heshima imepungua, kuna watu wanaongea ya uongo madhabahuni kuna Nabii mmoja  amejigamba hivi karibuni kuwa Yesu atakaporudi atapanda gari lake jipya atamchukua toka kiwanja cha ndege na kwenda katika ibada kanisani kwake hii haiko sawa. kuwaombea mabaya viongozi fulani fulani ili either wafe, wapate ajari hiyo si kazi ya ukristo kazi yetu kuwatakia na kuwaombea amani wote wabaya kwa wazuri.
  • Kuthamini mambo mengine ya kidunia na kuyapa kipaumbele kuliko ibada ni kosa baadhi ya mambo kama vile Mapenzi, starehe, kazi na majukumu yetu ya kila siku

Mungu ni Mungu wa walio hai wenye uwezo wa kufanya ibada, Mungu si Mungu wa wafu  kwa maana hiyo basi ni vizuri kutengeneza mahusiano mazuri na Mungu wakati ukiwa bado hai, siku tutakapo kuwa tupo jenezani au kaburini tutakuwa hatuna sifa tena ya kuwasilana na Mungu safari itakuwa imeishia hapo. Haijalishi kama watu watakao kuwa hai watamsihi Mungu akupunguzie adhabu au akusamehe. Hakuna mtu yeyote duniani wa kuweza kumgeuza Mungu mawazo yake analotaka ndo huwa au hutokea. Haijalishi ni  Maaskofu, mashehe, Mapadre, maimamu, hata kiwe cheo gani ili mradi ni mwanadamu Mungu ni Mungu na mwandamu ni mwanadamu tu, na udongoni tutarudi tutake tusitake ndo Mungu alivyokwisha sema katika maandiko yake. (Mwanzo 3:19 Kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi)

 

Kuna tabia imeenea miongoni mwa baadhi ya watumishi wa Mungu wasiomjua Mungu aliye hai ya kugoma kwenda kushiriki baadhi ya ibada za mazishi hasa iwapo itajulikana kama marehemu alikufa vibaya kwa kukamatwa ugoni, kunyongwa, au kujinyonga, kunywa sumu, kumeza vidonge au kujiua kwa makusudi kwa namna yeyote ile. Lengo la kuu la kwenda kufanya ibada kwenye mazishi yeyote ni kupeleka injili ya Yesu Kristo kwa watu wote, kuna watu hawahudhulii ibada za kwenye nyumba za ibada kabisa lakini nafasi kama hizi ni fursa ya pekee ya kwenda kulitangaza jina la Yesu Kristo kwa kila kiumbe. Maandiko matakatifu yanatusisitiza kupeleka injili kwa kila kiumbe aamniye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa. (Marko mt 16:15-16 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa)

 

Kugoma, kutokwenda kufanya ibada ni kuhukumu huko, kama wakristo hatutakiwi kuhukumu hilo ni jukumu la Mungu mwenyewe (Mathayo mt 7:1 Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi) Kama Yesu mwana wa Mungu aliye hai, aliwahi kuletewa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi na mashuhuda watu wazima walioshuhudia tukio lenyewe hakumuhukumu, wewe ni nani hata ufanye hukumu? Huna uovu wewe? (Yohana mt 8:3 – 11 Waandishi na Mafarisayao wakamleta mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati…                                                                                             

 

Vile vile Mungu huyu huyu Mtakatifu hapendi yeyote apotee bali wote waifikie toba. (2Petro 3:9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba). Vile vile Mungu hakufurahii kifo chake mwenye dhambi (Ezekieli 33:11-12 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya akaishi.Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa,Enyi nyumba ya Israeli?)

 

Ukizingatia hizi ni siku za mwisho  zilizotabiriwa ni lazima injili ihubiriwe kwa kila njia iliyopo na kwa gharama yeyote ile, ili kukamilisha kusudi la Mungu alilolikusudia, siku hizi kuna njia, vyombo vingi ambavyo kwavyo injili ipitie Youtube, Whatsapp, Twitter, snap chart, Tick Talk, google, Face book, Instagram, Telegram, WeChat na Pinterest na nyingine nyingi, vyote hivyo ni vibebeo vya injili ya Kristo tunapaswa kuvitumia, maana maeneo yote hao kuna viumbe. Mungu wetu ni tajiri vyote ni mali yake dunia na wote wakaao ndani yake.

 

BAADHI YA FAIDA/MANUFAA YA KUFANYA IBADA AMBAYO NI KUMCHA BWANA

1. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunaongeza siku za kuishi (Mithali 10:27Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasiohaki itapunguzwa”)

2. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunafungua mlango wa maarifa (Mithali 1:7Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa , Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.) (Danieli 1:17-20 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza, mbele ya mfalme Nebukadreza. Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania na Mishaeli na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.)

3. Kufanya ibada, kumcha Bwana kuna imarisha umoja wetu na Mungu, kwa kawaida mwanadamu anapokuwa mbali na Mungu anakuwa mpweke, na mnyonge na kukosa furaha ya kweli.Siku za nyuma katika nchi yetu swala la ibada lilipewa kipaumbele sana, ilikuwa kila shule inajipangia siku mojawapo katika wiki inaweza kuwa Jumatano au ijumaa kila mtoto ataenda kwenye dhehebu lake analoabudu japo kwa masaa kadhaa, siku hizi yamepungua sana au hayapo kabisa kwa baadhi ya shule kama shule itakuwa sio ya kimishenary. Mkazo uliopo sasa hivi ni watoto kufaulu kwa kiwango cha A. Binafsi mimi nimekulia katika ibada za shuleni tangu udogo. Ukimpa mtoto malezi ya dini sio rahisi ayaache atakapokuwa mtu mzima  (Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee) kila mtu ana uhitaji wa kufanya ibada hata wafungwa waliopo gerezani wanatakiwa wapatiwa nafasi ya kufanya ibada kulingana na imani yake, hilo ni hitaji kuu la moyo wa mwanadamu yeyote mwenye pumzi ya uhai.

4. Kufanya ibada, Kumcha Mungu kutakupelekea kupata uzima wa milele (Mithali 14:27 “Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, ili kuepukana na tanzi za mauti”)

5. Kufanya ibada, kumcha Mungu unapata hekima (Zaburi 111: 10 Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa zake zakaa milele.

6. Kufanya ibada, kumcha Bwana ni ulinzi kwako na watoto wako (Mithali 14:26 Kumcha Bwana ni tumaini imara; watoto wake watakuwa na kimbilio.)

7. Kufanya ibada, kumcha Bwana ni utajiri (Mithali 22:4 Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.)

8. Kufanya ibada, kumcha Bwana kunatupa nguvu ya kuangusha ngome na vifungo vya adui (Marko mt 9:28-29 Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? . Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.)

9.   Anayependa ibada hata akipata changamoto yeyote hawezi toka nje mstari akamkosea Mungu Mfano Ayubu, Abrahamu na mkewe na changamoto ya kutopata mtoto mapema, Danieli na wenzake. Kuna vita katika maisha yako hautaweza kushindana nayo mpaka utakapoamua kuwa mtu wa ibada.

10. Kufanya ibada kunaleta majibu ya maswali ya maswali mbali mbali yanayotutatiza Roho Mtakatifu msaidizi wetu mkuu hawezi kutuaacha katika kila hali tunayopitia, mitego yote ya siri huteguliwa hata katika ulimwengu wa roho, hakuna jambo jambo gumu la kumshinda Mungu.

 

Kiuhalisia haitakiwi kuegemea kwenye siku moja katika wiki bali kila siku ni siku ya kumfanyia Mungu wetu ibada, Ni kosa sana kuegemea katika siku sahihi ya kweli kufanya ni Jumamosi au Jumapili tu, Mungu anatakiwa kufanyiwa ibada kila siku iitwayo leo. Kwa sababu rehema zake kila siku ni mpya basi basi na tumsifu, tumshukuru, tumwombe, tumwabudu, tumfanyie ibada, tumpende, tumwimbie, tumtolee sadaka kila siku.

Sio kila mtu anafaa kuongoza ibada, sio kila mtu ni mtumishi wa madhabahuni kumtumikia Mungu sio lazima kusoma elimu ya juu sana kama PHD na kadhalika ni wale waliokubaliwa na Mungu mwenyewe na mtu wa kuongoza huwa anakuwa na kibari kutoka kwa Mungu ukimwona tu huulizi sio kazi kama ya watu wa duniani. Kwa kuwa ibada ni ya Mungu mtakatifu mwenyewe kwa hiyo hata waongozaji Mungu hujitafutia mwenyewe kwa kuomba uongozi wake na msaada kutoka kwa Roho Mtakatifu wake. Wote wanaolazimisha kawaida wataona huduma ni ngumu sana, maana watatumia akiri na usomi wao, usipate msukumo wa kufanya ibada sababu ya changamoto fulani inayokusibu maishani baadhi ya changamoto ni kukosa kazi, kustaafu na uchumi kuyumba, ugonjwa mkubwa usioponyeka kirahisi, kukosa mchumba nk, bali ibada inatakiwa iwe ni sehemu ya utaratibu wako wa maisha.

Pia ni kosa kufanya ibada za wafu, hiyo ni kufanya ibada za mizimu, kukaribisha mashetani katika maisha yako shetani hana urafiki na mtu yeyote, unaweza sema mbona baadhi ya watu wanafanikiwa kwa nguvu nyingine? Hawa watu utajiri waupatao una masharti magumu kiasi ambacho hupelekea kujutia maishani na moto wa jehanamu wa milele unawasubiri baada ya maisha haya mafupi ya hapa duniani. Shetani hafanyi kitu kwa hasara. Ni kama kuku anayelishwa vizuri amewekwa tayari kwa ajiri ya sikukuu inayokuja. Hapa pia kuna watu wanajiita watumishi wa Mungu lakini wanatumia nguvu nyingine ole wao, Mungu aonaye sirini anawaona kweupee. Wanawapotosha watu wasimjue Mungu wa kweli pia wamchukie Mungu.

Asili ya ibada na vitu vyote vinavyoambatana na ibada ni Mungu mwenyewe. Vitu vinavyoambatana navyo ni Sadaka na Ngoma

SADAKA

Aliyetoa sadaka njema na ya thamani kuliko wote ni Mungu Mtakatifu mwenyewe, na sadaka inatofautiana uzito, aliyetoa sadaka ya kuku au njiwa si sawa na aliyetoa sadaka ya ngombe.

(Yohana mt 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.) Hata katika Kitabu cha Mwanzo walipoumbwa Adamu na Hawa Mungu alitoa sadaka. (Mwanzo 3:21 BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Pia kuna baadhi ya watu waliwahi kufanya mdhaha na kipengele hiki cha ibada (Matendo yaMitume 5:1-11  Anania na Safira Mungu alivyowaadhibu hadharani.

 

NYIMBO/SIFA/NGOMA

Asili ya ngoma, nyimbo, sifa ni mbinguni malaika wanamuimbia Mungu usiku na mchana bila kuchoka, kuna muimbaji mmoja aliwahi kuuliza swali “mziki asili yake wapi?” Mziki asili yake ni mbinguni.

Habari za mbinguni nyingi zimefichwa ingawa kitabu cha ufunuo kwa sehemu kimetudokezea kidogo (Ufunuo wa Yohana 4:8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.

Mziki na dansi tulizo nazo leo duniani shetani amekopi na ku paste kutoka kwa Mungu Mtakatifu yeye si unajua alikuwa karibu na Mungu mno. (Ezekiel 28:14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; name nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.

Kati ya huduma tuzifanyazo hapa duniani ambayo itakuwa na muendelezo mpaka mbinguni ni uimbaji wa kumsifu Mungu wetu.Tutamsifu bila kuchoka tukiwa na miili mipya ya mbinguni. Naamini utakuwa umejifunza kitu, asante kwa kuchukua muda kujifunza ujumbe wa neno la Mungu endelea kujifunza kupitia masomo mengine

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
             wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
             (Waebrania 10:25).
       4.    Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo  ( 2Thesalonike                        3:10)
       5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
       6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
              anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
              Barikiwa na Bwana


               Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
                injiliyajioni@gmail.com
              www.injilijioni.blogsport.com

              
             
   


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


Wednesday, June 19, 2024

USIJITENGE

(Mhubiri 4:9-12 Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliyepeke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?Hata ikiwa mtu aweza kumshinda Yule aliye peke yake,wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.)

Mstari huo hapo juu pia baadhi ya wachungaji au watumishi wanaofungisha ndoa hupenda kuutumia kwa ajili ya wanandoa ni makosa kuutumia huu mstari ni kama unabariki watu kuwa wawili, katika ndoa tunabariki mke na mume kuwa mwili mmoja, kuwa pamoja katika shida na raha kuwa kitu kimoja ndo lengo la Mungu wakati anaumba mwanamke na mwanaume. Kuwa pamoja huku hakutakiwi kupungua hata mtoto au watoto watakapo patikana kama wanavyofanya baadhi ya wanandoa, mapenzi kuhamishia kwa mtoto waliopewa na Mungu.

Injili ya mtakatifu inasisitiza kuhusu katika ndoa kuwa mwili mmoja (Mathayo 19:6  Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe)

Kama Mkristo na msafiri sio vizuri kukaa peke yako, peke yako, kuna kuchoka, kukata tamaa, kukatishwa tamaa. Katika maisha ya ukristo tunatakiwa lazima kushirikiana na wengine ili kuongeza joto la imani, ili kukua kiroho na kustawi, shetani ana mitego na hila nyingi bila msaada wa Mungu, ambaye mara nyingine Mungu huweza kumtumia jirani yako au mwenzako ili kukupatia baadhi ya majibu ya maombi yako, unaweza kujiuliza hivi kwa nini Mungu kuomba niombe mimi majibu ampe mwingine, Mungu mambo yake mengine anavyoyafanya hatutakiwi kuuliza, kuhoji hoji sana yeye ni mfinyanzi sisi ni udongo tu. (Warumi 9:21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?)

Haijalishi una kila kitu mwana wa Mungu ili kupata ushindi katika maisha ya ukristo lazima kushirikiana na wengine hata madhehebu ambayo hawatofautiani sana na wewe au hawapingani na haki za ubinadamu pamoja na sheria za nchi husika, pamoja kuwa tuna utofauti wa kimadhehebu Mungu anayajua yote na anatukubari, anawakubari wote ambao hawavunji sheria, Mungu hata katika uumbaji wake ameumba watu wenye tofauti tofauti wanene, wembamba, wafupi, vilema, vipofu, wakali , wapole lakini wote anatusikiliza halafu hatubagui, Mvua, Jua  anatupatia sote. JAMBO LA KUJIULIZA Mbona Mungu yeye ana kila kitu tena nchi na vyote viijazavyo ni  mali yake lakini pamoja na hayo yote aliyokuwa nayo anafanya kazi pamoja na MALAIKA, WANADAMU, MUNGU MWANA, NA MUNGU ROHO MTAKATIFU. 

(Warumi 8:28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.) na (Yohana Mtakatifu 17:11 Wala mimi simo tena ulimwenguni, nami naja kwako.Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.)

Mungu katika kuumba hii dunia hakuumba dunia peke yake maandiko yanasema (Mwanzo 1:26 Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani.) Tena hakuumba kitu kimoja ameumba mbali mbali samaki wapo wa aina mbali mbali, wanyama wapo wa aina mbali mbali, maua yapo ya aina mbali mbali, watu hivyo hivyo wapo tofauti tofauti.

Tena kuna mahali katika biblia pameandikwa vitu vyote ni watumishi wake (Zaburi 119:91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.)

Haijalishi una misuri ya imani ya jinsi gani ni kanuni moja wapo ya ushindi katika ulimwengu wa roho ni kuwa na mwingine ili kubebana katika roho.

YESU MWANA WA MUNGU hakufanya kazi peke yake alikuwa na wanafunzi kumi na mbili nao walikuwa wanafanya kazi  wawili wawili ili kutiana moyo , YESU alikuwa akitiwa moyo (Luka Mtakatifu 10:1 Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.) na Mungu na Roho Mtakatifu, pamoja na Malaika hakuwa peke yake, kuna kipindi alikuwa anakumbana na vitu vya kukatisha tamaa vya kumfanya arudi nyuma akawa akitiwa moyo ili aendelee na safari. Bwana Yesu kabla ya kuzaliwa kulikuwa na manabii wengi wametabiri ujio wake, nabii anapotabiri lazima Mungu pia atamsukuma, au atamwongoza katika kuomba kwa ajili ya hilo alilooneshwa, lakini pia kuna watumishi Mungu aliwaambia kuwa hawatakufa kabla ya kumuona masihi wa Bwana 

(Luka mt 2:25 - 32 Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu,jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumuona Kristo wa Bwana.Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani,ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,  Yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako,Kwa amani, kama ulivyosema;  kwa kuwa macho yangu yameona wokovu wako,uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,  kuwa utukufu wa wa watu wako Israeli.) 

Hii inathibitisha kuwa Yesu hakufanya kazi peke yake kabla na hata baada ya kuzaliwa. Ila pia ujue yaliyoandikwa katika biblia ni baadhi ya mambo sio kila kitu kime nakiliwa, kama kingeandikwa kila kitu kilichofanyika biblia ingekuwa ni kitabu kikubwa mno kisicho bebeka. (Yohana Mtakatifu 21:25 Kuna mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.)

ROHO MTAKATIFU hafanyi kazi peke yake anashirikiana na wanadamu katika kufanya mapenzi ya Mungu Baba anashirikiana na Yesu Mwana wa Mungu.

Mungu baba yeye ni Mweza yote anaweza kufanya kila kitu peke yake na kikatokelezea vizuri tu anaweza kuumba vyoote sababu yeye ni mweza yote, angeweza kuumba dunia peke yake kwa siku moja kufanya vyote kwa siku moja ashindwi jambo.

Mungu huwa anabariki mtu anapokuwa na mwingine (Mathayo 18:20 Kwa kuwa walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu nami nipo hapo hapo kati kati yao.)

Hata utendaji wa karama za Roho Mtakatifu hufanya vizuri zaidi kunapokuwa na watu wengine sio kifichoni, sababu utendaji wa karama au kazi za Roho Mtakatifu lengo ni kumtukuza Mungu mbele ya watu wake.

Hata watumishi wenzetu waliotutangulia walifanya kazi wawili au watatu sio kila mtu kivyake vyake

1. Paulo alikuwa karibu na Silla. (Matendo ya Mitume 16:25 Lakini panapo usiku wa manane Paulo         na sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa                    wengine walikuwa wakiwasikiliza) 

2. Samweli alitumika chini ya kuhani Eli. (1Samweli 3:1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA        mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.)

3. Eliya alikuwa pamoja na Elisha (2Wafalme 2:4 Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha;         maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, kama BWANA aishivyo, na roho             yako iishivyo, sitakuacha.Nao wakafika Yeriko.)

4. Musa alitumika pamoja na Haruni. (Kutoka 7:1 BWANA akamwambia Musa, Angalia,                         nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii         wako.)

5. Esther na Mjomba wake Mordekai. (Esther 2:7 Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti         wa mjomba wake kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri     na uso mwema; naye walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa naye         binti yake yeye.) 

6. Daniel alikuwa na akina Shadraka, Meshaki na Abednego. (Danieli 2:17-18 (Ndipo Danieli, akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Anania na Mishaeli na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa Mbinguni kwa habari ya siri hiyo ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.)

Binafsi wakati nipo mdogo nilipomaliza tu elimu yangu ya msingi sikuchukua muda mrefu nilikuwa nikiishi na bibi yangu mzaa mama, huyu bibi  alikuwa ni mtu wa maombi, sala na kuhudhuria kanisani ni bibi ambaye kwa kweli Mungu amekuwa akimtumia katika mambo fulani fulani. Kwa hiyo na mimi nikawa na kopi na ku paste. Mara kadhaa nilikuwa nakosea kosea lakini akawa ananinyoosha wewe fanya hivi. Kipindi kile ndo nikawa pia nimeanza kusikia na kuona vitu katika ulimwengu wa roho, nilipokuwa nikiona kitu nikawa namwuliza bibi mbona nikiomba naona vitu hivi na hivi ? akawa akinitia moyo na kuniambia hapo maana yake Shetani amedhurika nikawa nasonga mbele kwa hiyo tangu udogo mpaka sasa hivi nimekuwa mara kadhaa nikawa naona vitu katika ulimwengu wa roho, sisemi ili kujifagilia kujifanya wa kiroho saaana kuliko wengine hapana, vitu hivi mara nyingi nimekuwa nikiviona sababu yake kubwa ni kuombea tukio, hali au mtu husika. Ili mwisho wa siku Mungu wa Israeli apate utukufu anao stahili kupitia utendaji kazi wa Roho Mtakatifu.

Ukikaa peke yako ni rahisi shetani kukurushia kombora likakupata, likakudhuru.Kombora la shetani likirushwa kwako target yake ni Wewe mwenyewe, mtoto wako, mke wako au mali zako akipiga kimojawapo amekupiga wewe.

Kwa hiyo watu wa Mungu pamoja na makwazo au migogoro ambayo inaweza kutokea kwenye kanisa lolote lile hapa duniani, sisi sote ni binadamu sio malaika, kusameheana na kutulia katika kanisa ambalo Mungu anatukuzwa na wanaamini katika biblia takatifu ni muhimu. (Waebrania 10:25 Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.)

Kuwa pamoja ni umoja ambao Mungu anautarajia kutoka kwetu, tukiwa pamoja tunafananishwa na kuni zinazowaka kwa umoja huwa zinatoa moto vizuri, lakini ukiutenga ukuni uwake peke yake basi mara moja utazimika na moto wake kuishia.

Kila binadamu aliyeumbwa na Mungu ni kiungo na ni mtumishi wa Mungu na ana sehemu katika mwili wa Kristo, sisi kama viungo katika mwili wa Kristo hakuna kiungo cha kuzauliwa kila kiungo cha mwili ni cha muhimu sana ili kufanikisha kusudi la Mungu la kuwepo kwetu hapa duniani mwingine anakuwa Kahaba, au Mlevi au muuaji wa kupitiliza vyote tabia zote chafu Mungu ana kusudi naye. Rahabu pamoja na ukahaba wake Mungu alikuwa na mpango naye kukamilisha kusudi lake (Yoshua 2:1-24 Yoshua mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko...) Paulo pamoja na kuua walokole enzi zile Mungu alikuwa na mpango naye (Matendo ya mitume 9:7 -20 Na wale watu waliokuwa wakisafiri pamoja naye wakasimama kimnya, wakiisikia sauti wasione mtu...)

Sio hivyo tu Mungu anapotugawia karama zake lengo lake ni kulijenga, kuhudumia kanisa Mungu hagawi karama ili uitie mfukoni uitumie peke yako, na karama za Mungu zinafanya kazi vizuri zaidi kwenye umoja na pia hapo Mungu hupata utukufu wake anao stahili yeye peke yake.

Tukio la kweli si la kubuni

Kuna Mpendwa mmoja siku moja akiwa anaendesha gari lake huku akiwa hajatia lock, mwanawe wa kiume alikuwa amekaa upande wa pili wa dereva kwa  bahati mbaya akafungua mlango gari likiwa linatembea haikuwa kwenye spidi kubwa sana sababu ya ubovu wa bara bara lakini mtoto alitoka nje ya gari, huyu mama akasimama ghafla akijua kuwa amesha mkanyaga mwanawe wa kumzaa, akawa amesimama hawezi kuendesha gari akijua kuwa ameshaua, mara mtoto akainuka toka pale chini barabarani,  alipodondoka akawa akijifuta  futa vumbi hakuuawa.Baada ya kuadithia mwenyewe mzazi huyu wa kike kilichotokea, kesho yake jioni binafsi nikiwa nimerudi nyumbani kutoka kazini nabadilisha nguo, chumbani kwangu niliona live katika ulimwengu wa roho sufuria na mafiga matatu, kwa juu usawa wa kama mita mbili toka nilipokuwa nimesimama ndani ya chumba changu Sikuelewa maana yake ila baada ya kumwuliza Roho Mtakatifu nikapata tafsili yake, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu nikaona kilichokuwa kinapikwa kwenye ile sufuria, ilikuwa ni vipande pande vya karatasi vimeandikwa kwa ajili ya manuizo mbali mbali kwa ajili ya familia hii, kingine cha ajabu ambacho wakati mwingine namshangaaga Mungu ni kuona tukio hili karibu mwaka mmoja kabla na likitokea namna ya kuomba ili kuzuia lisije leta madhara kwa familia husika, Sijui Mungu alikuwa anataka kuwafundisha nini hii familia, ina kauwezo uwezo fulani hivi, tukafanya maombi maalumu ya kuvunja vunja na kuharibu mipango na manuizo yote ya shetani kwa hii familia, wanaendelea vizuri na afya njema mpaka leo hii,kwa kuwa Mungu wetu ni mkuu kuliko mungu wa dunia hii (1Yohana 4:4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.) Mungu akajipatia Utukufu.  ila pia tukio hili limewafanya wawe na uchaji na Mungu sio kama huko nyuma.

Ikumbukwe kuwa Shetani akirusha Mshale wa kwanza ukikukosa atarusha mwingine hakatagi tamaa haraka. Kama kwa Yesu Mwana wa Mungu aliyehai alijaribiwa zaidi ya Jaribu moja, wewe ni nani usijaribiwe? kwenye biblia maandiko yanasema Yesu alijaribiwa kwa majaribu matatu kiukweli haiwezekani siku zote hizo 40 Yesu ajaribiwe kwa majaribu matatu tu. Shetani anapofanyakazi yake huifanya kwa ufanisi zaidi anapoifanya kwa mtu aliye peke yake.

Hata katika documentary za wanyama wanaokula nyama utaona kama kuna sehemu kuna Mto wenye MAMBA, wanyama wakipita kundi, mamba anavizia aliye peke yake peke yake hathubutu kuingia kati anakaa pembeni amkamate aliye peke yake. Kama yupo nchi kavu atajitahidi amvutie kwenye maji au mtoni ili amtafune vizuri.

Hata mnyama SIMBA AU CHUI anapokimbiza Mnyama humkimbiza mnyama humkomalia aliye peke yake atamkimbiza mpaka ampate amkabe shingoni akose pumzi, afe aanze kumla.

Ndo hivyo hivyo Shetani afanyavyo kazi yake huifanya kwa ufanisi zaidi mtu anapokuwa peke yake, na hata kanisa au watu wa Mungu wanapokuwa hawana umoja huo ni mtaji kwa shetani, ahimidiwe Mungu kwa Roho wake Mtakatifu tunaweza kujikuta tunafanya kazi kwa umoja yeye Roho akiwa kiunganishi.

Hata mtu ambaye anayehubiri au kufundisha, kuombea wahitaji kawaida huwezi kufanya wewe peke yako lazima Umruhusu Roho Mtakatifu awe mwalimu na msaidizi ukiomba msaada wake anakusaidia usipohitaji msaada wake basi atakuacha upambane na hali yako.Halafu mwisho wa siku mambo yana kuwa ni magumu ila ukimruhusu Roho Mtakatifu akuongoze mambo ni marahisi mno unateleza tu kama mlenda.

Tunayaweza mambo yote katika yeye atutiaye nguvu Wafilipi (4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.)

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
             wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
             (Waebrania 10:25).
       4.    Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo  ( 2Thesalonike                        3:10)
       5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
       6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
              anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
              Barikiwa na Bwana


               Mtumishi Emmanuel T.M.Omari
                injiliyajioni@gmail.com
              www.injilijioni.blogsport.com

              
             
   


Tuesday, January 30, 2024

KUUKOMBOA WAKATI








(Efe 5:16 - 17 Mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.)

Unapoishi hapa duniani usiishi kihasara hasara, jitahidi uulize kwa Mungu kwa watu kwa marafiki lengo kuu ujue kusudi la wewe kuwepo hapa duniani, kama utakuwa hujui kusudi la wewe kuwepo hapa ndo biblia ina hasa tusiwe wajinga, bali werevu kwa kujua kusudi la kuwepo hapa duniani, kila mtu ana kusudi la yeye kuumbwa haijalishi unapitia vikwazo gani.

Mtoto anapozaliwa kwanza anatokea katika ulimwengu wa roho huko mbinguni, Mungu huwa kuna kuwa na jambo ameshaliandaa litokee duniani (Yeremia 1:5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.)

Kusudi kuu la Mungu kumuumba Binadamu ni ili amuabudu na kumtumikia Mungu. Mungu akikupatia saa 24 ndani yake kuna muda kwa ajili yake ambao si chini ya 2:40 haijalishi hali ya maisha ni ngumu.

Siku yenye masaa 24, dakika 1440 na sekunde zake 86,400 na wiki yenye siku 7

Kuna vitu Mungu anavifanya wewe mwenyewe unatakiwa ujiongeze uelewe maana yake, Mfano: (Isaya 66:1 BWANA Asema hivi, mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu,)

Mungu miguu yake ameiwekea duniani, angeweza kuweka sayari nyingine hakuna mtu wa kuweza kuhoji, lakini ameweka duniani binafsi huwa nashukurugi kwa uwepo wa Mungu kupitia miguu yake, miguu yake ni ni ulinzi tosha dhidi ya mwovu na waonezi wengine. Na ni baraka tosha

Na muda ukipita, potea haurudi tena (Mathayo Mt 26:40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akawaambia Petro , Je ! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?. sehemu nyingine katika Biblia inasema ombeni ili msiingie majaribuni.)

Ili ushinde majaribu , usiingie mtegoni, usiingie katika matatizo, mitego ipo mingi shetani aliyotuandalia hatutakii mema hata kidogo na hakubali kushindwa akishindwa hili ataandaa jingine ili mradi tu atupate. Anakaa vikao kila siku siku kupanga afanye nini kwa wakristo au awafanyie nini Wakristo, baadhi ya waombaji wanaweza kushiriki hata hata vikao vya kuzimu bila ya Shetani kujua, jinsi Mungu alivyo wa ajabu.

Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote, Ukishaingia kwa Yesu unakuwa ni mmoja kati ya wenye haki kuna changamoto nyingi, kuna vikwazo vingi lakini ahimidiwe Mungu yeye huweza kutuponya na yote hayo.

Tupo duniani hapa ili kuukomboa wakati na jitahidi mwana wa Mungu usitumie muda mwingi sana katika mambo yanayopoteza muda sana, tutumie kwa kiasi, mfano matumizi ya Facebook,Whatsapp,Tv na moves zake katika series Twitter, Tick talk, Istragram.

Kuna baadhi ya Movie, CD Moja ina picha,au videos 100 au zaidi nani leo anao muda wa kuangalia movie, muda wote huo kazi utafanya saa ngapi ? muda ukiupoteza nani atakulipa? Kwa hiyo wapendwa tuwe makini sana, maana lengo lake moja wapo ni la kutupotezea muda tukiwa hapa duniani, tujione kuwa tuna muda mrefu sana wa kufanya mambo mbali mbali.

Usiipende sana dunia inaweza ikakumeza ukapotelea huko (1Yohana 2:15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia.Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.)

Roho Mtakatifu anaweza kuongea na wewe usielewe hali kama hii ilimtokea Farao, Mungu alitumia masuke saba membamba na masuke saba mema na Ngombe saba wema na ngombe saba dhaifu, ndoto imekuja tofauti tofauti lakini muhusika hakuilewa ilibidi aitwe mfungwa Yusufu, naye kwa Msaada wa Mungu akatafsili ndoto na kuweza kuponya Taifa na mataifa na ukimwengu kwa jumla. (Mwanzo 41:14-16  Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.Yusufu akamjibu Farao, akasema, si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.)

Unapokuwa na muda wa kumsifu, kumwomba, kumwabudu Mungu fanya hivyo tumia muda wako vizuri wewe unao huo Muda ujue ya kuwa wakati wewe unauchezea huo muda kuna mtu yupo gerezani hawezi kuomba kwa uhuru sababu ya mazingira, mwengine yupo ICU, mwingine yupo mochware, mwingine nchi zao hazina amani, mwingine analishwa na mpila, mwingine anapumulia machine, mwingine baada ya muda mchache Mungu ameridhia afe tu sababu hata akiongezewa muda wa kuishi hatakuwa na jambo la maana. Muda wake wa kuishi hapa duniani umeisha aondoke  akasubirie hukumu huko mbele ya safari.

Mungu huwa anatushangaa sana iwapo tuna muda wa kula tena mara tatu kwa siku ila hatuna muda wa kusoma na kuomba, tuna muda wa kutumia na wenzi wetu, na watoto wetu na marafiki wetu, tuna muda wa kufanya kazi zetu ila muda muda wa kutumia simu ila muda na yeye Mungu tunaukosa  na yeye tunaukosa wakati masaa 24 tumepewa.Mbona wengine wanaweza kupata muda wa kuongea na Mungu wakati wote tunapewa masaa 24 kwa siku?

Kama watu wengine wanapoteza muda kwenye kucheza karata, bao, draft, vilabu vya pombe, kubet, waache waendelee usiwaangalie we angalia ratiba zako na usikose kuwa na muda wa kumpa yeye aliye kupa uzima. (Mithali 1:10 inasema Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali.)

Muda ni zaidi ya fedha, ukipoteza fedha unaweza ukaipata tena ila muda ukiupoteza sio rahisi kuupata tena muda uleule, ukikupita umepita. Wengi wetu tupo makaini sana na matumizi ya fedha lakini sio matumizi ya muda, kuna watu unaweza kuwasikia wakiongea “ ah !!! tupo tupo hapa kidogo tunapoteza muda”

Kama wakristo hatutakiwi kujua kwamba Yesu bado atachelewa kurudi bali mfalme wa wafalme Bwana wa Majeshi amekaribia mno yupo mlangoni tunatakiwa tuwe na utayari tukijua ya kuwa Bwana Yesu Kristo wakati wowote kuanzia sasa anarudi kuja kutuchukua kanisa (watu wake walio mwamini tu)

(Ufunuo 12:12 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari ! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.)

Tumuombe Mungu hata Serikali au viongozi wasiwe mawakala wa kutupotezea muda, muda unaweza kupotea kwa namna mbali mbali, Mfano baadhi ya tawala katika nchi za wenzetu hazisimamii vizuri matengenezo ya bara bara unafanya wananchi wapoteze muda bara barani, hospitalini zisipoboreshwa na madaktari kuwezeshwa wananchi wanaweza kuwa wanasotea huduma hizo muda mrefu, kwa hiyo tuziombee serikali zinazosimamia vizuri na kwa haki zidumu na kudumu. Misafara ya viongozi unakuta akipita rais foleni tena mnasimamishwa kabla ya muda, waziri fulani msafara, mkuu wa majeshi msafara,

Kuna Makesi yapo mahakamani wala hazikutakiwa kufika mahakamani mfano kesi ya mtu na jirani yake kugombea mpaka labda futi 3 au  tu ishawahi kutokea kesi ikanguruma miaka 10 yote hii ni kupotezeana muda mara kesi inatajwa mara inaahirishwa siku zinaenda, muda unapotea, muda ukipotea haurudi, kesi inaisha inakatwa rufaa inaaza tena moja.

Tuwe na ratiba za kufanya mambo yetu kwa ajili ya maendeleo yetu binafsi na ya wenzetu, kama Wakristo tusiwe sababu ya kupoteza muda wa watu wengine kwa kuwazungusha kuna baadhi ya ajira zinatangazwa nafasi chache mfano nafasi 2 tu lakini watu watakao kuja kuomba kazi husika huweza kufika hata 100 sasa hapo kuna nini, mbaya zaidi ukute mazingira mengine yameshatembea na inajulikana kuwa yupi atayechukua hiyo nafasi basi inakuwa ni changamoto kweli.

Ishawahi tokea hapa hapa kwetu Tz benki fulani walioajiliwa wengi wao ilikuwa ni majina ya watoto wa viongozi walioshika madaraka nafasi za juu juu ingawa sawa lakini unaweza ukajiuliza kwa nini inakuwa hivyo lakini majibu ya uhakika sio rahisi kuyapata.

Kila jambo linawakati wake na Mungu ni mpangaji wa mambo yote na Shetani ndo mvurugaji wa mipango yote, kuna baadhi ya mambo Mungu anaweza kuwa ameshajibu ila shetani anaweza kuchelewesha majibu kama ilivyotokea kwa Daniel Mtu wa Mungu (Daniel 10 : 12 - 14 Ndipo akaniambia, Usiogope,Daniel; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.

Tuwe makini sana na vitu vinavyotupotezea muda, hata tukakosa muda wa kuwa faragha na Mungu wetu, Mungu huwa anapenda ushirika, urafiki na wanadamu,(Mwanzo 3:8-9 Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga;Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone.BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?) pia Mungu ni Mungu mwenye wivu, haoni hasara kuingilia kati na kukupokonya kile ambacho kinakupotezea muda na kumkosesha ushirika na yeye.

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
             wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
             (Waebrania 10:25).
       4.    Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo  ( 2Thesalonike                        3:10)

       5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
       6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
              anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
                                                                                                     Ni mimi
Mtumishi Emmanuel T. M.Omari

injiliyajioni@gmail.com
www.injilijioni.blogsport.com