(Mhubiri 4:9-12 Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliyepeke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?Hata ikiwa mtu aweza kumshinda Yule aliye peke yake,wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.)
Mstari huo hapo juu pia baadhi ya wachungaji au watumishi wanaofungisha ndoa hupenda kuutumia kwa ajili ya wanandoa ni makosa kuutumia huu mstari ni kama unabariki watu kuwa wawili, katika ndoa tunabariki mke na mume kuwa mwili mmoja, kuwa pamoja katika shida na raha kuwa kitu kimoja ndo lengo la Mungu wakati anaumba mwanamke na mwanaume. Kuwa pamoja huku hakutakiwi kupungua hata mtoto au watoto watakapo patikana kama wanavyofanya baadhi ya wanandoa, mapenzi kuhamishia kwa mtoto waliopewa na Mungu.
Injili ya mtakatifu inasisitiza kuhusu katika ndoa kuwa mwili mmoja (Mathayo 19:6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe)
Kama Mkristo na msafiri sio vizuri kukaa peke yako, peke yako, kuna kuchoka, kukata tamaa, kukatishwa tamaa. Katika maisha ya ukristo tunatakiwa lazima kushirikiana na wengine ili kuongeza joto la imani, ili kukua kiroho na kustawi, shetani ana mitego na hila nyingi bila msaada wa Mungu, ambaye mara nyingine Mungu huweza kumtumia jirani yako au mwenzako ili kukupatia baadhi ya majibu ya maombi yako, unaweza kujiuliza hivi kwa nini Mungu kuomba niombe mimi majibu ampe mwingine, Mungu mambo yake mengine anavyoyafanya hatutakiwi kuuliza, kuhoji hoji sana yeye ni mfinyanzi sisi ni udongo tu. (Warumi 9:21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?)
Haijalishi una kila kitu mwana wa Mungu ili kupata ushindi katika maisha ya ukristo lazima kushirikiana na wengine hata madhehebu ambayo hawatofautiani sana na wewe au hawapingani na haki za ubinadamu pamoja na sheria za nchi husika, pamoja kuwa tuna utofauti wa kimadhehebu Mungu anayajua yote na anatukubari, anawakubari wote ambao hawavunji sheria, Mungu hata katika uumbaji wake ameumba watu wenye tofauti tofauti wanene, wembamba, wafupi, vilema, vipofu, wakali , wapole lakini wote anatusikiliza halafu hatubagui, Mvua, Jua anatupatia sote. JAMBO LA KUJIULIZA Mbona Mungu yeye ana kila kitu tena nchi na vyote viijazavyo ni mali yake lakini pamoja na hayo yote aliyokuwa nayo anafanya kazi pamoja na MALAIKA, WANADAMU, MUNGU MWANA, NA MUNGU ROHO MTAKATIFU.
(Warumi 8:28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.) na (Yohana Mtakatifu 17:11 Wala mimi simo tena ulimwenguni, nami naja kwako.Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.)
Mungu katika kuumba hii dunia hakuumba dunia peke yake maandiko yanasema (Mwanzo 1:26 Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani.) Tena hakuumba kitu kimoja ameumba mbali mbali samaki wapo wa aina mbali mbali, wanyama wapo wa aina mbali mbali, maua yapo ya aina mbali mbali, watu hivyo hivyo wapo tofauti tofauti.
Tena kuna mahali katika biblia pameandikwa vitu vyote ni watumishi wake (Zaburi 119:91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.)
Haijalishi una misuri ya imani ya jinsi gani ni kanuni moja wapo ya ushindi katika ulimwengu wa roho ni kuwa na mwingine ili kubebana katika roho.
YESU MWANA WA MUNGU hakufanya kazi peke yake alikuwa na wanafunzi kumi na mbili nao walikuwa wanafanya kazi wawili wawili ili kutiana moyo , YESU alikuwa akitiwa moyo (Luka Mtakatifu 10:1 Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.) na Mungu na Roho Mtakatifu, pamoja na Malaika hakuwa peke yake, kuna kipindi alikuwa anakumbana na vitu vya kukatisha tamaa vya kumfanya arudi nyuma akawa akitiwa moyo ili aendelee na safari. Bwana Yesu kabla ya kuzaliwa kulikuwa na manabii wengi wametabiri ujio wake, nabii anapotabiri lazima Mungu pia atamsukuma, au atamwongoza katika kuomba kwa ajili ya hilo alilooneshwa, lakini pia kuna watumishi Mungu aliwaambia kuwa hawatakufa kabla ya kumuona masihi wa Bwana
(Luka mt 2:25 - 32 Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu,jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumuona Kristo wa Bwana.Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani,ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, Yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako,Kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameona wokovu wako,uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, kuwa utukufu wa wa watu wako Israeli.)
Hii inathibitisha kuwa Yesu hakufanya kazi peke yake kabla na hata baada ya kuzaliwa. Ila pia ujue yaliyoandikwa katika biblia ni baadhi ya mambo sio kila kitu kime nakiliwa, kama kingeandikwa kila kitu kilichofanyika biblia ingekuwa ni kitabu kikubwa mno kisicho bebeka. (Yohana Mtakatifu 21:25 Kuna mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.)
ROHO MTAKATIFU hafanyi kazi peke yake anashirikiana na wanadamu katika kufanya mapenzi ya Mungu Baba anashirikiana na Yesu Mwana wa Mungu.
Mungu baba yeye ni Mweza yote anaweza kufanya kila kitu peke yake na kikatokelezea vizuri tu anaweza kuumba vyoote sababu yeye ni mweza yote, angeweza kuumba dunia peke yake kwa siku moja kufanya vyote kwa siku moja ashindwi jambo.
Mungu huwa anabariki mtu anapokuwa na mwingine (Mathayo 18:20 Kwa kuwa walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu nami nipo hapo hapo kati kati yao.)
Hata utendaji wa karama za Roho Mtakatifu hufanya vizuri zaidi kunapokuwa na watu wengine sio kifichoni, sababu utendaji wa karama au kazi za Roho Mtakatifu lengo ni kumtukuza Mungu mbele ya watu wake.
Hata watumishi wenzetu waliotutangulia walifanya kazi wawili au watatu sio kila mtu kivyake vyake
1. Paulo alikuwa karibu na Silla. (Matendo ya Mitume 16:25 Lakini panapo usiku wa manane Paulo na sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza)
2. Samweli alitumika chini ya kuhani Eli. (1Samweli 3:1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia BWANA mbele ya Eli. Na neno la BWANA lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.)
3. Eliya alikuwa pamoja na Elisha (2Wafalme 2:4 Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha.Nao wakafika Yeriko.)
4. Musa alitumika pamoja na Haruni. (Kutoka 7:1 BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako.)
5. Esther na Mjomba wake Mordekai. (Esther 2:7 Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; naye walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa naye binti yake yeye.)
6. Daniel alikuwa na akina Shadraka, Meshaki na Abednego. (Danieli 2:17-18 (Ndipo Danieli, akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Anania na Mishaeli na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa Mbinguni kwa habari ya siri hiyo ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.)
Binafsi wakati nipo mdogo nilipomaliza tu elimu yangu ya msingi sikuchukua muda mrefu nilikuwa nikiishi na bibi yangu mzaa mama, huyu bibi alikuwa ni mtu wa maombi, sala na kuhudhuria kanisani ni bibi ambaye kwa kweli Mungu amekuwa akimtumia katika mambo fulani fulani. Kwa hiyo na mimi nikawa na kopi na ku paste. Mara kadhaa nilikuwa nakosea kosea lakini akawa ananinyoosha wewe fanya hivi. Kipindi kile ndo nikawa pia nimeanza kusikia na kuona vitu katika ulimwengu wa roho, nilipokuwa nikiona kitu nikawa namwuliza bibi mbona nikiomba naona vitu hivi na hivi ? akawa akinitia moyo na kuniambia hapo maana yake Shetani amedhurika nikawa nasonga mbele kwa hiyo tangu udogo mpaka sasa hivi nimekuwa mara kadhaa nikawa naona vitu katika ulimwengu wa roho, sisemi ili kujifagilia kujifanya wa kiroho saaana kuliko wengine hapana, vitu hivi mara nyingi nimekuwa nikiviona sababu yake kubwa ni kuombea tukio, hali au mtu husika. Ili mwisho wa siku Mungu wa Israeli apate utukufu anao stahili kupitia utendaji kazi wa Roho Mtakatifu.
Ukikaa peke yako ni rahisi shetani kukurushia kombora likakupata, likakudhuru.Kombora la shetani likirushwa kwako target yake ni Wewe mwenyewe, mtoto wako, mke wako au mali zako akipiga kimojawapo amekupiga wewe.
Kwa hiyo watu wa Mungu pamoja na makwazo au migogoro ambayo inaweza kutokea kwenye kanisa lolote lile hapa duniani, sisi sote ni binadamu sio malaika, kusameheana na kutulia katika kanisa ambalo Mungu anatukuzwa na wanaamini katika biblia takatifu ni muhimu. (Waebrania 10:25 Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.)
Kuwa pamoja ni umoja ambao Mungu anautarajia kutoka kwetu, tukiwa pamoja tunafananishwa na kuni zinazowaka kwa umoja huwa zinatoa moto vizuri, lakini ukiutenga ukuni uwake peke yake basi mara moja utazimika na moto wake kuishia.
Kila binadamu aliyeumbwa na Mungu ni kiungo na ni mtumishi wa Mungu na ana sehemu katika mwili wa Kristo, sisi kama viungo katika mwili wa Kristo hakuna kiungo cha kuzauliwa kila kiungo cha mwili ni cha muhimu sana ili kufanikisha kusudi la Mungu la kuwepo kwetu hapa duniani mwingine anakuwa Kahaba, au Mlevi au muuaji wa kupitiliza vyote tabia zote chafu Mungu ana kusudi naye. Rahabu pamoja na ukahaba wake Mungu alikuwa na mpango naye kukamilisha kusudi lake (Yoshua 2:1-24 Yoshua mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko...) Paulo pamoja na kuua walokole enzi zile Mungu alikuwa na mpango naye (Matendo ya mitume 9:7 -20 Na wale watu waliokuwa wakisafiri pamoja naye wakasimama kimnya, wakiisikia sauti wasione mtu...)
Sio hivyo tu Mungu anapotugawia karama zake lengo lake ni kulijenga, kuhudumia kanisa Mungu hagawi karama ili uitie mfukoni uitumie peke yako, na karama za Mungu zinafanya kazi vizuri zaidi kwenye umoja na pia hapo Mungu hupata utukufu wake anao stahili yeye peke yake.
Tukio la kweli si la kubuni
Kuna Mpendwa mmoja siku moja akiwa anaendesha gari lake huku akiwa hajatia lock, mwanawe wa kiume alikuwa amekaa upande wa pili wa dereva kwa bahati mbaya akafungua mlango gari likiwa linatembea haikuwa kwenye spidi kubwa sana sababu ya ubovu wa bara bara lakini mtoto alitoka nje ya gari, huyu mama akasimama ghafla akijua kuwa amesha mkanyaga mwanawe wa kumzaa, akawa amesimama hawezi kuendesha gari akijua kuwa ameshaua, mara mtoto akainuka toka pale chini barabarani, alipodondoka akawa akijifuta futa vumbi hakuuawa.Baada ya kuadithia mwenyewe mzazi huyu wa kike kilichotokea, kesho yake jioni binafsi nikiwa nimerudi nyumbani kutoka kazini nabadilisha nguo, chumbani kwangu niliona live katika ulimwengu wa roho sufuria na mafiga matatu, kwa juu usawa wa kama mita mbili toka nilipokuwa nimesimama ndani ya chumba changu Sikuelewa maana yake ila baada ya kumwuliza Roho Mtakatifu nikapata tafsili yake, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu nikaona kilichokuwa kinapikwa kwenye ile sufuria, ilikuwa ni vipande pande vya karatasi vimeandikwa kwa ajili ya manuizo mbali mbali kwa ajili ya familia hii, kingine cha ajabu ambacho wakati mwingine namshangaaga Mungu ni kuona tukio hili karibu mwaka mmoja kabla na likitokea namna ya kuomba ili kuzuia lisije leta madhara kwa familia husika, Sijui Mungu alikuwa anataka kuwafundisha nini hii familia, ina kauwezo uwezo fulani hivi, tukafanya maombi maalumu ya kuvunja vunja na kuharibu mipango na manuizo yote ya shetani kwa hii familia, wanaendelea vizuri na afya njema mpaka leo hii,kwa kuwa Mungu wetu ni mkuu kuliko mungu wa dunia hii (1Yohana 4:4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.) Mungu akajipatia Utukufu. ila pia tukio hili limewafanya wawe na uchaji na Mungu sio kama huko nyuma.
Ikumbukwe kuwa Shetani akirusha Mshale wa kwanza ukikukosa atarusha mwingine hakatagi tamaa haraka. Kama kwa Yesu Mwana wa Mungu aliyehai alijaribiwa zaidi ya Jaribu moja, wewe ni nani usijaribiwe? kwenye biblia maandiko yanasema Yesu alijaribiwa kwa majaribu matatu kiukweli haiwezekani siku zote hizo 40 Yesu ajaribiwe kwa majaribu matatu tu. Shetani anapofanyakazi yake huifanya kwa ufanisi zaidi anapoifanya kwa mtu aliye peke yake.
Hata katika documentary za wanyama wanaokula nyama utaona kama kuna sehemu kuna Mto wenye MAMBA, wanyama wakipita kundi, mamba anavizia aliye peke yake peke yake hathubutu kuingia kati anakaa pembeni amkamate aliye peke yake. Kama yupo nchi kavu atajitahidi amvutie kwenye maji au mtoni ili amtafune vizuri.
Hata mnyama SIMBA AU CHUI anapokimbiza Mnyama humkimbiza mnyama humkomalia aliye peke yake atamkimbiza mpaka ampate amkabe shingoni akose pumzi, afe aanze kumla.
Ndo hivyo hivyo Shetani afanyavyo kazi yake huifanya kwa ufanisi zaidi mtu anapokuwa peke yake, na hata kanisa au watu wa Mungu wanapokuwa hawana umoja huo ni mtaji kwa shetani, ahimidiwe Mungu kwa Roho wake Mtakatifu tunaweza kujikuta tunafanya kazi kwa umoja yeye Roho akiwa kiunganishi.
Hata mtu ambaye anayehubiri au kufundisha, kuombea wahitaji kawaida huwezi kufanya wewe peke yako lazima Umruhusu Roho Mtakatifu awe mwalimu na msaidizi ukiomba msaada wake anakusaidia usipohitaji msaada wake basi atakuacha upambane na hali yako.Halafu mwisho wa siku mambo yana kuwa ni magumu ila ukimruhusu Roho Mtakatifu akuongoze mambo ni marahisi mno unateleza tu kama mlenda.
Tunayaweza mambo yote katika yeye atutiaye nguvu Wafilipi (4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.)
" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.
Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.
1. Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
2. Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
3. Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
(Waebrania 10:25).
6. Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).
Mtumishi Emmanuel T.M.Omari