Monday, July 24, 2023

MANABII WA UONGO



(Mathayo Mtakatifu 24:11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi).

Neno la Mungu lipo wazi limetahadharisha kutokea kwa Manabii wengi wa uongo na kudanganya wengi, sio manabii tu, wachungaji, watu wa maombezi, Watumishi wa Mungu,Wahubiri, makuhani, Maaskofu, Mitume, Waalimu hizi ni nyakati za kukaa vizuri na Mungu wako pia si wakati wa kuwa vugu vugu ni heri uwe moto au baridi, ukiwa vugu vugu ni rahisi sana kusombwa na mafuriko. (Ufunuo wa Yohana 3:15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto). Hizi ni siku za Mwisho kila mtu anatakiwa awe makini na awe macho kweli kama wateule wameambiwa wawe macho, itakuwaje kwa watu wasio wateule?

  (Mathayo Mtakatifu 24:24 Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.)

Cha ajabu hawa wanaojiita watumishi wa Mungu kwa matendo  yao si watumishi wa Mungu aliye hai, maana kama wanaombea watu walioumbwa na Mungu na kuwadai POSHO  tuwaulize kwa andiko lipi au ni lini Yesu aliombea mtu, au mitume wapi waliwahi kuombea mtu wakadai posho, na kama mtu hakutoa posho hakupata maombi aliyostahili Kuweka posho kidogo ya wastani mfano ;5000/= Roho Mtakatifu na akuongoze katika hili  (kwa huduma changa, ila huduma ikiwa imekua inaweza kuwekwa kikapu na watu wakawa wakichanga kwa jinsi ya watakavyoguswa  sio mbaya  ili kuiwezesha huduma kukua, kununua au kukarabati viti vya huduma, kumuwezesha mtumishi naye  kama binadamu aweze kukidhi mahitaji ya familia yake naye ana watoto, mke au mume ,kulipia TRA vibali n.k, kulipia umeme,kulipia maji, mtumishi naye anatakiwa avae vizuri yeye na familia yake  ila kucharge gharama ya 200,000/= au 300,000/= kumuona mtumishi tu, haijakaa sawa. Maisha ya siku hizi sio kama ya zamani siku hizi kila kitu pesa, huwezi sema unaenda alummiun Africa kampuni ya mabati ukaombe bati kwa ajili ya kuwezesha wahitaji wakae pazuri, Au uende kampuni ya Bakresa ukaombe akupatie maji ya bure kwa ajili ya washirika wako, hiyo kitu haiwezekani  (Mathayo Mt 10:8 Pozeni wagonjwa, fufueni wafu,takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure). Kuna jumbe Yesu aliwaambia wanafunzi wake kipindi kile kutokana na mazingira ya wakati ule ilikuwa sahihi, ila kwa mazingira ya sasa tuliyonayo inabidi kujiongeza. Kumalizia kipande hicho kuna sehemu imeandikwa Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Jiulize unaweza kwenda benki bila utaratibu ukachukue mi hela kwa sababu ni mali ya BWANA?

Kama tunatakiwa kulipia Mungu angetuambia tulipie pumzi ya uhai ni tajiri yupi leo angeliweza kulipia? Ulizia wagonjwa wanaolazwa na kuhitajika wawekewe oxygen gharama yake ni kubwa mno unaweza kuta lisaa limoja gharama yake inaweza zidi hata milion moja,   Mungu wetu Muumba wa mbingu na nchi anatufanyia vitu vingi mno bure kabisa Ulinzi, Uhai, pumzi, Amani, uwezo wa kuongea, kusikia, viungo vya miili yetu vilivyo ndani ya mwili na vilivyo nje ya mwili kufanya kazi yake ipasayo vizuri tu, hatulipii kutokana na makosa yetu, anatuwazia mema siku zote (Yeremia 29:11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi.Asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu)

Mbona wengine wanamkosea Mungu na Mungu aliye hai hawaadhibu?, anawaacha tu, Mungu wetu mkuu ni mpole sana lakini pia ni mkali sana, kwa hiyo ni lazima tumpende tumuheshimu na pia tufate maagizo na miongozo  yake. Bila yake yeye hatuwezi kumshinda huyu mwovu shetani , kwani shetani ana nguvu zaidi yetu pasipo msaada wake Mungu. Mungu hamlazimishi mtu yeyote kumfuata yeye, alishaongea mara nyingi kwa kutumia vinywa vya watumishi wake mbali mbali akitaka wote tumfuate Yesu ili tupone, tuokoke. Hatutaki? Je unataka ashuke toka Mbinguni mwenyewe ili wewe ufanye maamuzi ya kuokoka' kumkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi? Sasa kwa taarifa yako Mungu hatashuka Ng'o ili kukushawishi wewe umwamini Ukikubari umepona na ukikataa hukumu ya milele inakusubiri.Chaguo ni lako binafsi kumfuta Yesu au wengine unaowajua na kuwaamini wewe.

Ingawa Mtumishi wa Mungu hupimwa kwa matendo, lakini haijalishi mtumishi anafanya wema fulani mf.kutoa pesa, kusaidia wahitaji,anaponya wagonjwa, anatenda miujiza, anafufua wafu, anatoa mapepo, anafukuza wachawi, hatumpimi mtumishi wa Mungu kwa jambo moja tu au mawili, lazima tumkague kwa mambo mengine pia ili aweze kufaulu mtihani, hata maandiko yametuasa kuwa tusiziamini kila roho bali tuzijaribu , maana manabii wengi wa uongo walitokea, wametokea na watatokea.

(1Yohana Wapenzi, msiimini kila roho, bari zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.)

Viroja/Vituko vya manabii wa uongo

1.    Ukilipa fedha nyingi unaombewa sana ukitoa kidogo unaombewa kidogo, kwa lugha                               nyingine kwenye nyumba za ibada hizi matajiri wanaombewa zaidi kuliko masikini.

2.    Manabii wa uongo hawa wanatumia chumvi, sabuni, pete maalum,bangili, cheni, mafuta, maji,                stika, picha zao binafsi  vyote hivyo sio bure bure.

3.  Baadhi ya hawa manabii wanataka waabudiwe, wasujudiwe sifa ambazo anayestahili kuzipata ni             Mungu  peke yake.

4.  Baadhi ya hawa mitume hawa wa uongo wanachezea viungo nyeti vya baadhi ya akina mama                  ambao  ni wake za watu  wanaopitia changamoto mbali mbali katika maisha. Mf.kukosa watoto,             kutokuwa   na kazi.  Wanajifananisha na Madaktari wa kawaida ambao wakati mwingine huweza           kumkagua  mgonjwa, sehemu mbali mbali za mwili wake ili kumuondolea, kujua shida fulani                 inayomsibu.                                                                                          

5.    Baadhi ya watumishi hao manabii wanasumbua wafuasi wao wakisema kwa kuwa wao ni                       watakatifu waliopo duniani kwa hiyo hawapaswi kukanyaga adhi iliyo jaa dhambi.Kwa hiyo                   wabebwe juu juu wanapohubiri na wanapoombea wagonjwa.

6.    Kwenye makanisa ya nchi za jirani waumini wanachapwa viboko kama njia mojawapo ya kutoa           mapepo. Huko huko kuna baadhi ya watumishi wanasumbua waumini wao wakitaka wanunuliwe            magari ya kifahari sana kwa kuwa Mungu ni tajiri. Sehemu nyingine waumini walifungiwa                   milango, taa zikazimwa mahekaru yakachomwa moto maelfu ya watu wakafa.

7.    Kuna mwingine namjua, kwa macho nimemwona alikuwa ana agua kwa kutumia mizimu, ila hivi         karibuni nilionana naye tena  mwenyewe kabisa akaniambia sasa hivi anaendelea na kuagua ila               anatumia biblia.Na wateja, waumini lukuki kila siku jioni anawaombea wagonjwa, pia anawaza             kupanua wigo wa huduma yake maana wateja wamekuwa wengi mno.

8.    Uwe makini sana na mjuzi wa neno la Mungu ukisaidiwa na Roho Mtakatifu bila hivyo ni ngumu           kuwatambua, ukifika kwenye makanisa yao utakuta nao wanataja taja kuwa siku hizi kuna                       manabii wa uongo wengi tuwe makini sana.

9.   Wanapoombea wagonjwa, wateja wao baadhi ya hawa watumishi huwakanyaga wahitaji au wenye           shida  au kuwachapa fimbo kama njia moja wapo ya kuagua au kutoa mapepo na majini.

10. Huweza hata kudhalilisha muumini anaye muombea mfano: Kumdhalilisha muumini au mteja                mwenye tatizo la kukojoa kitandani kwa kusema wewe unakojoa kitandani hadharani, wakati kwa          hekima tu ungeweza kumfanyia kwa faragha, ili kumlinda mteja na sio hivyo mnamdhalisha na              wewe kubeba sifa na utukufu.

Kila kukicha watumishi wapya na mafunuo mapya wanazuka, na style zao za kiutumishi na style zao za maombezi inayowapelekea watu kuzubaa na kubweteka katika kutegemea maombi ya watumishi kila siku wakati suala ala maombi ni jambo linalomuhusu kila muumini. Kama maandiko yanavyosisitiza tusikome kuomba na sio tusikome kuombewa. (1the 5:17 ombeni bila kukoma;)

Maandiko yapo wazi yakisema ole wake wa yule apotoshaye, anayesababisha makwazo (Luk 17:1 Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake !)

Sio kweli kuwa manabii, watumishi wa kweli hawapo ila katika watumishi hao hao wengine ni wa uongo, na changamoto iliyopo ni  asilimia kubwa ya watu hawana muda wa kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kusoma na kuelewa, neno la Mungu  hivyo basi inapelekea watu wengi kujikuta wameingia kwenye mkumbo wa Manabii,watumishi hao wa uongo. Na maandiko yapo wazi hayakupepesa macho kwa habari ya tahadhari, maandiko yameonya kuwa. Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.)

Hawa watumishi wa uongo yote wanayoyafanya wanaongozwa na babayao aliye baba wa uongo (Yohana Mt 8:44 Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa ya baba yenu ndio ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa ni mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na babaa  wa huo.)

Ukimfuata shetani na kumtumikia siku ya mwisho itakapofika utahukumiwa pamoja naye katika ziwa la moto, maandiko yapo wazi (Mathayo Mt Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto,Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari ibilisi na malaika zake;)

Wewe unamfuata nani? nani mwanzilishi wa imani yako sasa kwa taarifa yako kule alikoenda, alikoishia muasisi wa imani yako alipo ishia ndipo na wewe utakapoishia ukifuata kwa bidii. Ila pia kwa kusoma maandiko tunaambiwa hakuna jina jingine tulilopewa la wokovu ila ni moja tu, ni Yesu Kristo pekee, utake usitake.(Matendo ya mitume 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.)

Injili ya kweli msisitizo mkubwa ni watu kuacha dhambi kumgeukia Mungu na kuokoka, kukombolewa kitu ambacho hata malaika mbinguni hushangilia (Luka mtakatifu 15:7 Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu) na hayo mengine ya mwilini tutajaliziwa. Na huo ndio msingi mkubwa ili kumsaidia mtu kumponya mwili na roho, na kumfundisha muumini ajue jinsi ya kutotegemea watu, mtu au vitu bali Mungu pekee aliye kila mahali. 

Ukimfuata Mungu na kumtumikia  siku ya mwisho ikifika Yesu atakaporudi lazima akuchukue siku ya unyakuo ikifika, kama Yesu alivyoahidi na kusisitiza kuwa mbingu na nchi zitapita lakini maneno yake hayatapita kamwe.

Kimbilia kwa Yesu haraka kipindi hiki una uhai, ukifa itakuwa hamna nafasi tena ya kutengeneza, tengeneza na Mungu wako sasa hujui ya kesho imepangwa nini kwako. Mithali 27:1 Usijisifu kwa ajili ya kesho; kwa maana hujui yatakayo zaliwa na siku moja.

Kila mmoja atasimama yeye peke yake na Mungu kutoa hesabu ya matendo yake alipokuwa duniani, wazazi hawatajibia watoto, wala watoto hawatawajibia wazazi (Warumi 14:12 Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.)

Enyi manabii wa uongo nawasihi acheni kuwapotosha watu wa Mungu, Mungu anawaona  uganga mnaotumia na kuwahadaa na kupata pesa zina mwisho. Itakusaidia nini uwe tajiri na mali mengi  fedha, magari, majumba harafu uikose mbingu? (Mathayo 16:26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara  nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?)

Hata ipigwe kelele vipi, Manabii, Watumishi, waalimu, maaskofu, mitume, wainjilisti, wachungaji wa uongo wataendelea na kuongezeka, kama maandiko matakatifu yalivyotabiri kabla.

Siku hizi kumekuwa na watumishi wengi waliojiingiza katika utumishi na kufanya kazi ya Mungu ni kama ajira mbadala na sio kazi ya wito, inafananishwa na kazi ya  mshahara, wanasimamia andiko (1Wakorintho 9:14 Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo injili).Hofu ya Mungu inapotea taratibu. Asilimia kubwa ya watu wanaokosa ajira, hujiingiza kwenye utumishi wa Mungu,Uchungaji, uaskofu, unabii, ila kwa mtazamo wa maandiko, swala la kushuhudia kila mtu amjue Kristo, ni jukumu la kila muumini, biblia haikusema watumishi wote tufungue makanisa na kujipachika ma vyeo na wake zetu  (Marko mt. 16:15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe)  unaweza kushiriki kwa kuingia moja kwa moja au hata kuchangia huduma hizo nawe kwa namna moja au nyingine utakuwa umeshiriki na umefanya ushuhudiaji, na una thawabu yako katika huo utumishi. Pia sio lazima wote tuwe wachungaji, maaskofu, manabii, waalimu,  fanya kwa upande wa kile ulichobarikwa, nacho, unaweza kusaidia kazi ya Mungu katika maeneo mbali mbali nawe ukawa una fungu lako katika huduma husika. Amua kusimama na watumishi mbali mbali wa Mungu ili kuisukuma kazi ya Mungu, Duniani hapa tunaishi kwa utofauti tofauti, kuna watu Mungu anawatumia mno lakini hawana uwezo wa kuendesha huduma zao, sababu wana changamoto ya fedha, na wengine wana fedha za kumwaga, simama katika eneo hilo hilo saidia kazi mbali mbali za Mungu ili Mungu apate utukufu pia nawashauri wamwombe Mungu awasaidie jinsi ya kuzitumia pesa kwa busara katika mapenzi yake, ili pia kupata ulinzi wa ki Mungu. Enzi za Yesu kulikuwa na watu ambao walikuwa na fedha zao mf.Yusufu Arimathaya, hakujitokeza mara kwa mara lakini Yesu alipokufa wanafunzi waliingiwa na hofu kuu, hawakuwa na ujasiri tena Mungu anamtumia Tajiri Yusufu Arimathaya (Mathayo mt 27: 57 Hata ilipokuwa jioni akafika tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;) (Sio lazima watu wote wawe miongoni mwa wanafunzi wa Yesu, lakini wanaweza kutumika sehemu fulani na thawabu yao haitawapotea Mungu ni mwaminifu)

Watu wengi wanavutiwa na huduma hizo za watumishi hao wa uongo, sababu moja inayopelekaa watu kila siku kumiminika ni miujiza na sio Yesu mtenda miujiza na baadhi ya hao manabii hutoa chakula cha mwilini mf,Mchele, soda Nyama, Sukari,etc bure  na ukisha ingia kwenye huduma hizi unashindwa kuchomoka labda neema ya Mungu ikupitie uchomoke na kulijua neno la Mungu.Maandiko yapo wazi yanaposema yawezekanaje kipofu kumwongoza kipofu mwenzie je hawatatumbukia shimoni wote wawili?

(Luka Mt 6:39 Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?)

Siku hizi kuna idadi kubwa ya watu hawahudhurii kabisa nyumba za ibada sababu ya viroja vinavyotokea kwenye nyumba za ibada na kukwaza mtu mmoja mmoja, mtu anaona ni kheli akae nyumbani tu kama akifa, atazikwa tu, nyumba za ibada sio mahali tena pa kutua mizigo bali ni sehemu ya kwenda kukusanya makwazo na kuongeza stress.

Watumishi hawa waliovaa mavazi ya kondoo wanapokuwa viongozi wakuu, makanisa wameyajenga kwa jitihada na uhamasishaji wao utawaambia nini? 'kama unakwazika sepa, Makanisa si yapo mengi?'

Watumishi hao mara nyingi wanapenda kukuza majina yao kuliko majina ya Mungu, utasikia kwa kiboko ya majini na wachawi, kwa babu wa upako, kwa mfalme wa wafalme miujiza ndo kitu kikubwa kinachowavutia, sisi binadamu ni watu wa ajabu unakimbilia miujiza wakati kila dakika ipitayo Mungu anakufanyia muujiza uwezo wa kuona, kutembea, kusikia,kuhisi, kuongea, kuwaza,,kupumua, kwenda haja kubwa au ndogo, kutafuna, kumeza, kutoa jasho, kusimama,  n.k kwa hiyo ni mtu wa miujiza anayetafuta muujiza na hamnaga waumini wa kudumu kwenye makanisa haya wengi ni watu wenye shida wanaotaka kuombewa, watatue shida za kimwili. 

Mwisho wa siku Mungu aliye hai, hatukuzwi na Shetani anafurahia fursa hizo maana huwa anazitafuta kwa udi na uvumba (Ayubu 2:1 Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhulisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhulisha mbele za BWANA). 

Pia kwenye kusanyiko la watu wa Mungu linapotokea afa mfano: Watu kukanyagana, moto, jengo kuporomoka, yaani afa lolote ambalo likapelekea watu wengi kufa, Fikiri mara mbili kwa nini afa litokee? mtumishi wa Mungu alikuwa wapi? kawaida mtumishi wa Mungu wa kweli huwa anaona mapema katika ulimwengu wa roho na ana uwezo wa kuzuia mapema kabla hayajatokea umwagikaji damu. Ukiona tukio limetokea afu ikachukuliwa bahati mbaya basi ujue, lilishapangwa hilo Amka utoke usingizini.

(Amosi 3:7 Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake)

Maana ya andiko hilo ni kuwa kwa kuwa Mungu wetu ni mkuu hakuna mwingine ila yeye peke yake ana uwezo wa kujua kila kitu kabla ya kutokea, iwe kibaya au kizuri. Kama kizuri atakujulisha na kama kibaya kuna namna fulani atakutaarifu mapema, ili uweze kuzuia kwa kutumia maombi, ili uweze kuepusha maafa na vifo. Kwa kuingia rohoni mapema na kupambana hadi ushindi upatikane, kwa kuwa Mungu ni mkuu, ushindi lazima utokee upande wa Mungu, na mtumishi wake mwisho wa siku Mungu apate utukufu, lakini ukiona tofauti, asomaye na afahamu. Sio hivyo tu ukisoma Ezekiel  18:32 Inasema (Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.) Sasa huyu anaye hua bira huruma, taarifa au tahadhari mapema ni Mungu au mungu? jibu wewe, Shetani kazi yake kuu ni kuua, kuharibu tangu mwanzo, hata kama atakufaidisha kuna mahali amekutegea, kama jogoo la Krismass unalipa chakula unajua siku yake utalichinja tu.

Ushuhuda/ushahidi

Kwa sisi tunaokaa Dar tunayaona mengi kuna mtumishi yupo anagawa upako wa kinabii anatoa mpaka number yake ya simu kwa gharama kidogo, ukishatoa pesa (sadaka) anakupa uwezo wa kumuwekea mtu mkono, kumnyoshea mkono muumini mkono anadondoka chini, ili uonekane una nguvu za ki Mungu sana, hicho mara nyingi kinawavutia watu na kuamini kuwa mtumishi husika ana tumiwa na Mungu.Ukiwa nabii una uwezo wa kumvuvia mtu umtakaye au watu uwatakao ili wakafanye miujiza ile ile inayofanywa na wewe kiroho upande giza inawezekana na kiroho upande wa nuru inawezekana, hamkumbuki kipindi kile Yesu alivyowatuma wale wanafunzi wake sabini na matokeo yaliyotokea? (Luk 10:17 Ndipo wale sabini waliporudi  kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako). pamoja na kuwa wote wanaomwamini Kristo wamepewa uwezo huo lakini pia kuna uwezekano wa kupoke special package. Kuna mawakala wa kishetani wanafuatilia baadhi ya watumishi wa Mungu ambao wanasumbua sana ufalme wao wakitaka waingie maagano nao ili wafanye kazi pamoja kwa ahadi ya kupewa msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo fedha lukuki, ili uwe maarufu fasta. Kuna baadhi ya watumishi walikuwa moto lakini sasa wamekuwa baridi, kuna baadhi ya hawa watumishi wametangulia mbele ya haki na wengine wapo hai bado, nahisi Mungu anawapa neema ya uhai ili wageuke na kutubu ila wasipoifanyia kazi nadhani Mungu anaweza kughairi.

Makanisa na yaendelee kuzuka tu maana imeshatabiliwa ila ole wao wasiomwamini Kristo na kuona kuwa Yesu hakufanya chochote kajipendekeza tu kutufia Msarabani, itawagharimu.Kitu kizuri kingine ni kuwa ukiwa na Roho Mtakatifu ukiingia kwenye blog, Youtube,facebook au  kuingia kwenye kanisa linaloongozwa na nabii au mtumishi asiye wa Mungu utapata signal tu na kujua kuwa huyu ni wa Mungu au mungu anayetawala madhabahu husika.

Ukifuatilia kwa undani watu wengi wanaofurika kwa Manabii, mitume, wa uongo na kutapeliwa ni Wakristo au waumini wa dini nyingine ambao hawana neno la Mungu (Biblia ) ndani ya mioyo yao na kuliishi.Pia ni wavivu wa kusoma na kufuatilia neno la Mungu aliye hai, Mtu unayelijua neno la Mungu huwezi kutapeliwa kizembe zembe na kuangukia kwenye majuto ambayo yanaweza kupelekea kuamini watumishi au Manabii wote ni matapeli wakati wapo wengi wazuri wanatabiri yanatokea na Mungu anatukuzwa.

Baadhi ya makanisa uwepo wake ni msukumo wa mtu au watu furani matajiri wenye pesa zao basi kanisa linazuka, kuna kanisa moja lipo Mbeya na miji mingine michache lenyewe linaruhusu wake wengi na kunywa  pombe nyingi ni sehemu ya ibada na lina waumini, siku nikipata jina lake nitakuja kulitaja hapa hapa.

Kawaida sisi kama binadamu kawaida ukitendwa mabaya, mfano umetapeliwa, umebakwa, umeumizwa utakuwa na chuki na watu wote waojiita Watumishi wa Mungu (kwa kutojua kupambanua kati ya watumishi wa Mungu muumbaji na watumishi wa mungu wa dunia hii) kitendo cha kuwachukia, kuwanenea maneno magumu, watu wanaojiita watumishi, ukiwachukia watumishi wa Mungu wa kweli unaweza kuingia katika mgogoro mwingine na Mungu aliye hai. (Mwanzo 27:29 Mataifa na wakutumikie na Makabila wakusujudie,Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako wakusujudie. Atakayekulaani alaaninwe, Na atakeyekubariki abarikiwe). ( Kwa imani sisi sote ni wana wa Ibrahimu). Kwenye biblia kuna kipindi Musa alioa mwanamke Mkushi,  Haruni na Miriam wakamteta Musa kwa kitendo chake cha kumuoa mwanamke Mweusi, kitendo hicho kilipelekea Miriam Kupata pigo kutoka kwa Mungu (Hesabu 12:1 - 15 Kisha Miriam na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya Mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana; alikuwa amemwoa Mwanamke Mkushi. Wakasema, Je ! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu ? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao. ... Sio hivyo tu unaweza ukawa na hasira na hata ya kuhudhuria ibada, ukaona ni mambo ya hovyo tu, usanii mtupu hata huyo Mungu mwenyewe sijui hata kama yupo si angezuia lisikutokee? Usiposhiriki ibada unavunja amri ya Mungu ya nne. Ukimkosea Mungu unakuwa umemfungulia, umemrahisishia Shetani kazi kukupiga vizuri. Ni kama vile mamba ili akushambulie vizuri uingie kwenye 18 zake uwe kwenye maji, sio nchi kavu.

Naomba niishie hapo lakini nataka ujue kuwa Shetani hajalala, halali akitutafuta ili tupotee na kwenda kwenye mauti ya milele pamoja naye, Mpendwa mkimbilie Yesu usije ukaingia kwenye moto wa milele aliowekewa Shetani na malaika zake walioasi.MKIMBILIE YESU LEO, USISUBIRI KESHO.

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
             wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
             (Waebrania 10:25).
       4.    Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo  ( 2Thesalonike                        3:10)
       5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
       6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
              anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).


                Ni mimi

Mtumishi Emmanuel T.M.Omari

injiliyajioni@gmail.com

www.injilijioni.blogsport.com





Thursday, April 27, 2023

SIFA ZOTE NI ZA MUNGU

 



Sifa ni somo lisilo na mwisho, na sifa zote anayestahili ni Mungu pekee na huyu Mungu amekaa katika sifa (Zaburi 22:3 Na wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.)

Mungu aliumba vitu vyote ili vimsifu yeye bahari inavyo vuma ni sauti ile inaenda kwa Mungu, duniani hapa hakuna sauti isiyo na maana, samaki kwa aina zao mbali mbali wanamsifu Mungu wanamuimbia, wanamuabudu yeye. Mungu anawasiliana na samaki (Yona 2:10 BWANA akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.)

 Miti ya aina tofauti tofauti inapovuma inatoa sauti mbali mbali zile ni sifa za Mungu anapokea, sisi binadamu hatuelewi ila Mungu mwenyewe anapokea sifa zake maana sifa  zake anayepokea ni  yeye mwenyewe. Miti ina uhai inasikia inatoa sauti tofauti tofauti (Mathayo mt 21:19  Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele.Mtini ukanyauka mara.) Upepo unapovuma tunausikia unatoka huku unaenda kule tunaona ni kitu cha kawaida unapovuma tunasikia sauti yake ni sauti ile inaenda moja kwa moja kwa Mungu anayestahili sifa peke yake anaelewa kitu gani kinazungumzwa. Mungu anaongeaga na upepo nao unamtii ndege warukao nao wanapoimba, wanamuimbia Mungu aliyeumba mbingu na nchi, Mungu ana namna anawasilana na ndege ushahidi wa andiko (1Wafalme 17:4 -6 Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.Basi akaenda akafanya kama alivyosema BWANA ; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha kerithi, kinachokabiri Yordan. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni  akanywa maji ya kile kijito), (Marko mt 4:41 41 Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?)

Hata ukiangalia dunia katika muhimili wake utagundua kuwa imeinama kidogo, kuinama ni kusujudu yeye Mungu anastahili sifa hizo peke yake. Pamoja na kuwa Mungu ameumba sayari zaidi ya moja, jua, mwezi na nyota, mbingu na nchi ameamua kuweka miguu yake duniani, lengo ni nini ili apate heshima yake, atukuzwe yeye peke yake. (Matendo ya Mitume 7:49 Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na Nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea ? Asema Bwana,)

Kwa hiyo ni wajibu wetu sisi sote tulioumbwa, wenye pumzi kumsifu yeye kama hatutaki basi mawe yatamsifu yeye. Na kiukweli kabisa hakuna mtu yeyote hapa duniani awe Askofu, Mtume na Nabii, Kuhani, Mchungaji, Shemasi, Mzee wa kanisa, Mwalimu, Mlokole na mtu yeyote Yule aliyepo na atakeyekuwepo anayeweza kumsifu Mungu ipasavyo ila Mungu anatuchukulia tu, anatubeba tu, inafanana na mtoto mdogo anayeita papa badala ya usahihi ni baba.

Hata Shetani wakati ule akiitwa Lucifer kule mbinguni hakuweza kumsifu Mungu ipasavyo na hakumwelewa Mungu kwa mapana yake ndo maana aliwaza kufanya kilichotokea (Isaya 14:13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano,) na akapata mshahara wake, hakuna asiyeujua.

Sifa zote ni za Mungu wetu ni kosa kubwa kwa binadamu kupokea sifa za Mungu (Isaya 42:8 Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.)


BAADHI YA WATU/MALAIKA WALIOJARIBU KUCHUKUA SIFA ZA MUNGU

  1. SHETANI Baba wa uongo

Ezekiel 28:14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; name nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati yam awe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi ; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; name nimekuangamiza , Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.  Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. Kwa wingi wa maovu yakokatika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, name nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.

 2.  MUSA NA HARUNI 

Mungu aliwapa maelekezo Musa na Haruni juu ya kupata maji ya kunywa  baada ya watu Kulalamika sana kwa ajili ya kiu wakiwa kulen Meriba Mungu alimwambia Musa awakusanye watu harafu auambie mwamba utoe maji, lakini Musa alifanya tofauti na maelekezo ya Mungu. Akamkorofisha Mungu. (Hesabu 20: 7 – 12 BWANA akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo,ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akatwaa hiyo fimbo kutoka mbele za BWANA kama alivyomwamuru. Musa ana Haruni wakawakusanya mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. BWANA akawaambia Musa ana Haruni, kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hmtawaingiza kusanyiko hili katika nchi ile niliyowapa.Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na BWANA, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kwao.)

3. HERODE

(Matendo ya Mitume 12: 21- 23 Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode alijivika mavazi ya Kifalme, akaketi juu ya kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababuhakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.) .

4. NEBUKADREZA

(Daniel 4: 28-33 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza. Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?  Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbai na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai,na kucha zake kama kucha za ndege.


BAADHI YA WALIOKATAA SIFA WAKARUDISHA KWA MUNGU HARAKA

  1. YESU MWANA WA MUNGU

(Luka 18:18 -19 Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?  Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja , naye ndiye Mungu.)

2.  PAULO NA BARNABA

Walikataa kata kata kupokea sifa anazostahili Mungu

(Matendo ya Mitume 14:11-15 

Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza suti zao, wakisema kwa kilikaonia,Miungu wametushuka kwa mfano ya wanadamu. Wakamwita  Barnaba, Zeu, na Paulo,Herme,kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.Kuhani wa Zeu ambaye hekaru lae lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume na Barnaba na Paulo,walipopata habari, wakararua nguo zao,wakaenda mbio                          wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,Wakisema, Akina bwana, mbona  mnafanya haya ?Sisi nasi ni wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema,ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai,aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.)

3.   PETRO NA YOHANA

Petro na Yohana walikataa kupokea sifa baada ya uponyaji wa kiwete

(Matendo ya Mitume 3: 11-12 11Basi alipokuwa aiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililo itwa tao la Sulemani, wakishangaa sana.12 Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi,kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa wetu sisi?)

MALAIKA WA MUNGU

(Mwanzo 32:24 - 29 Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri.Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvunguwa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka.Akasema, sikuachi, usiponibariki.Akamwuliza jina lako n'nani? Akasema,Yakobo.Akamwambia jija lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie,tafadhali,jina lako? Akasema, kwa nini waniuliza jina langu? Akamnabariki huko.)

Malaika aliyejitokeza kwa Yakobo katika umbile la binadamu, alipoulizwa jina lake hakutaka kabisa kujitambulisha jina lake.Kwa nini anakataa kutaja jina lake? Katika jina la mtu kuna kujulikana, au umaarufu kidogo. Mf.Ukiwa na simu aina ya  ya Sony na simu aina nyingine aina ya motorola au guava, automatic simu yenye jina ubora na viwango ni sony. Vile vile tunaona siku za hivi karibuni kumeibuka manabii wanaojitambulisha Manabii wakuu, au wanataja majina yao sana kuliko hata linavyotajwa jina la Yesu. Utasikia kwa Kiboko ya wachawi au kwa nabii...anayeponya wagonjwa ,jina linachukua sifa kwa asilimia fulani, ndio maana hata Malaika aliyetumwa na Mungu hakutaja jina lake, ni ameleta tu ujumbe alioagizwa na Mungu na kuondoka, hakuongeza na hakupunguza.

Ukuu wa Mungu hauelezeki tukimwelezea huwa anapokea kwa kutuchukulia ubinadamu wetu  (Isaya 66:1 1BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuwekea miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani ? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?)

(2 Mambo ya Nyakati 6:18 Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyojenga.)

Vitu vyote vilivyopo duniani vinamsifu Mungu Miti, Ndege, wadudu, nyota, mwezi, jua, bahari etc

Ni ngumu mno kuelezea sifa za Mungu ukijaribu kuelezea unaweza ukajikuta unaelezea matendo yake aliyotenda, anayotenda atakayotenda wakati yeye ni zaidi hayo yote.

Kabla ya kumuelezea Mungu jinsi alivyo jaribu kutafakari haya machache kwanza

Kama rehema zake ni mpya kila siku asubuhi utamwelezeaje huyu Mungu? (Maombolezo 3:22-23 Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi, Ni mpya kila siku asubuhi; uaminifu wako ni mkuu.)

(Yohana Mtakatifu 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele).Amemtoa mpendwa wake wa pekee, hana mwingine tena, amemtoa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi, tunaomkosea mara kwa mara, tunaomkasirisha mara nyingi, kwani kama angetupotezea tungelalamikia wapi? hapo upendo wake utauelezeaje?

(Isaya 6:2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.) Maserafi wamejifunika uso wasimuone Mungu wanaweza kumuelezeaje?

(Isaya 40:15 Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama kitu kidogo sana.)  Yaani nchi kama Tanzania yetu mbele zake Mungu ni kama kitone kimoja cha maji, visiwa anakinyanyua atakavyo, hapo Mungu utamwelezeaje?

Isaya 49:16 Inasema, Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbela zangu daima. Kama sisi binadamu wote duniani tumechorwa katika mkono wa Mungu, mkono wake ukubwa wake ni kama nini?

amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa na hakuna mtu aliyewahi kumuona unaweza kumuelezeaje huyu Mungu (1Timotheo 6:16  Ambaye yeye peke hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona.Heshima na uweza una yeye hata milele.Amina.)

Kila kiumbe, kuna viumbe wangapi duniani tofauti tofauti anavipa riziki, chakula chake utamwelezeaje huyu Mungu ? (Zaburi 136: 25 Kila chenye mwili akipa chakula chake; kwa maana fadhili zake ni za milele)

Kwa Wanyama Mungu anatambulika kama simba wa Yuda, kwenye miti yeye ni mti wa uzima, kwa yatima yeye ni baba wa yatima, kwa wajane yeye ni mume wa wajane, kwenye maji yeye ni maji yaliyo hai, kwenye miamba yeye ni mwamba imara, kwa wafalme yeye ni mfalme wa wafalme, kwenye mawe yeye ni jiwe kuu la pembeni, kwa wagonjwa yeye ni mponyaji, katika majeshi yeye ni Bwana wa majeshi, kwenye chakula yeye ni mkate wa uzima.etc

Kuna wimbo katika kitabu cha nyimbo Tenzi za rohoni no.3 unaitwa " Hata ndimi elfu elfu" hazitoshi kumsifu Mungu wetu niko ambaye niko.


BAADHI YA WANAOPOKEA SIFA ZA MUNGU BILA WOGA 

Dunia tunayoishi imejaa vituko visivyoisha na kadri tunavyoukaribia ujio wa Bwana Yesu Kristo mara ya pili hapa duniani mambo yanazidi ila ni Mungu mwenyewe atakayeingilia kati kumaliza yote haya. kuna watu wanapokea sifa za Mungu kwa kujua au kutojua na hawaogopi kwamba wafanyayo hayo ni dhambi kuna siku watakuja kuhukumiwa kwa hayo wanayofanya kama hawatatubu na kumrudia Mungu ni neema tu inayowabeba, hii neema kuna muda itafika mwisho.

Asilimia kubwa ya watumishi wanaogawa mafuta, chumvi, sabuni, wapo wengi tu Dar es salaam, Dodoma, Mwanza na wanapata wafuasi wengi kweli kweli, wanakubali kuabudiwa humo humo wapo wanaoitwa Wafalme wa wafalme mf.Zumaridi.Watumishi hawa wanafanya miujiza wanatumia jina la yesu, ila sio Yesu wa Nazareth, na kawaida wanatumia miungu yao kwa hiyo hata miujiza inapotendeka wanajipatia sifa kibao na mungu wao anainuliwa. Baadhi ya hawa wanaojiita watumishi wa Mungu wanaombea watu kwa pesa ukitoa nyingi unaombewa sana ukitoa kidogo unaombewa kidogo, wapo wengi na watazidi kwa sababu shetani yupo kazini na ukizingatia anajua kuwa ana muda mchache wa kufanya kazi, anapambana kupata wafuasi wengi ili ikiwezekana dunia nzima aitumbukize kuzimu Yesu akirudi aambulie patupu. Watumishi na manabii hawa wamekuwa wakitukuza majina yao, na kutajwa tajwa kuliko hata Mungu Mtakatifu.(Ufu 12:4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake). Wanafanana na baba yao aliyeasi jinsi anavyopenda misifa, ukisoma biblia utagundua idadi ya malaika walio asi mbinguni ni theruthi tu ya malaika, lakini nikikuuliza nitajie idadi ya malaika waasi ( mapepo) unaweza ukajaza hata kurasa nzima. Idadi ya malaika ambao hawajaa asi ni wengi zaidi lakini uliza majina yao kama tunavyosoma katika biblia unaweza ukasikia majina mawili au matatu tu, na walitaja majina kwa sababu maalum. Mfano Malaika aliyetumwa na Mungu aende kwa Mariam kwa ajili ya tukio kubwa la kuzaliwa kwa mtoto bila ya ushirika wa kimwili wa mwanamke na mwanaume.(Luka Mt 1:19 Malaika akamjibu akamwambia, mimi ni Gabriel, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema)

Jinsi ya kumsifu Mungu 

Tukitaka kumsifu Mungu vizuri turudi kwenye msingi wa neno la Mungu wenzetu waliotutangulia walifanyaje tumtazame Mfalme Daudi, mfalme aliyekuwa na Passion ya sifa tangia udogo wake wakati akichunga mifugo yao. Na kitabu cha Zaburi ni moja kati ya vitabu vya biblia Takatifu kinachoongoza kwa kuandika sifa za Mungu wetu. Tumsifu Mungu kwa kila tulichonacho kwa mdomo, makofi, kichwa, miguu, zeze, filimbi, gita, zeze, kinubi, ngoma, kelele, kinanda yaani kila kitu ulichonacho kinatakiwa kimsifu Mungu. (Zaburi 150:1 - 6 Soma  yote) (Zaburi 66 : 1 - 8 Soma) Kwa kawaida Shetani hapendi Mungu asifiwe ila hana uwezo wa kuzipokea sifa za Mungu na hawezi kukaa hata karibu yake anakimbia haraka sana alishafukuzwa zamani.Pia mwana wa Mungu usitoe machozi kwenye changamoto unazopitia bali ufurahi maana Mungu amekuamini, bali machozi yako yatoke na kububujika wakati unamwabudu Mungu Mtakatifu.

Pia ili kumsifu Mungu vizuri ni heli kuomba msaada wa Mungu Roho Mtakatifu mwenyewe bila yeye hatuwezi neno lolote (Yohana mt 4:23 Lakini saa inakuja, nayo saa ipo ambayo waabudu halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.)

Mziki, sifa asili yake ni mbinguni na tunatakiwa tumsifu Mungu katika kila hali sio tunapopita kwenye mema, au ushindi tu bali hata tunapopita kwenye changamoto mbali mbali tunatakiwa tumsifu  na kumshukuru Mungu wetu aliyehai. Tukiwa katika mapito hata yawe magumu Mungu yupo kila mahali tumkumbuke Ayubu, tumkumbuke Yesu Kristo Mwana wa Mungu tumkumbuke Paulo na Sila alipokuwa gerezani. Na tukiwa ndani ya sifa Mungu anaweza kufanya jambo. 

Sisi binadamu tumeumbwa kwa jinsi ya ajabu na ya kutisha, tupo tofauti tofauti hata tuwe mapacha, hata ukichukua vidole vyetu gumba na vingine havifanani,kila mtu ana kidole cha peke yake katika dunia hii haijalishi atazaliwa ulaya, jinsi Mungu alivyo wa ajabu. (Zaburi 139 :14 Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu na nafsi yangu yajua sana)

Ni nani anayeweza kumwelezea Mungu kwa uwezo wake ambao akili za kibinadamu zinagota katika kuelewa, tunabaki tunashangaa harafu hatuelewi (Ayubu 38:41 Ni nani anayempatia kunguru chakula, Makinda yake wanapomlilia Mungu awape chakula, Na kutanga tanga kwa kutindikiwa chakula ?)

(Zaburi 33:13 Toka mbinguni BWANA huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia) (Jaribu kuwaza Mungu amekaa eneo gani mpaka aweze kutuona binadamu woote duniani, kila mtu alipo haijalishi yupo eneo gani


Mwenyewe najijua kabisa siwezi kuelezea vizuri vile inavyopasa sifa za Mungu wetu hapa nimejaribu kuelezea kwa uchache kutokana na ufahamu wangu mdogo kwa jinsi Roho Mtakatifu alivyonijaria kwa sehemu. Somo hili haliishi na hata Mbinguni sifa hazitaisha hakuna usiku wala mchana kule ni sifa tu, hakuna kuchoka tukiwa na miili ya mbinguni ni furaha tu katika yeye. Barikiwa na Bwana.

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
             wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
             (Waebrania 10:25).
       4.    Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa                         agizo tangu kale, Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo  ( 2Thesalonike                        3:10)

       5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
       6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
              anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).

SOMO LINAENDELEA ...


     Ni mimi

Emmanuel T.M.Omari

injiliyajioni@gmail.com

www.injilijioni.blogsport.com