Tuesday, February 1, 2022

KUSAMEHE NA KUSAHAU

 




(Luk 17:3-4 Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.)

Kama utakuwa umekumbuka kuwa ulikosana na ndugu, jirani yako wakati mwingine kukumbuka huku ni Mungu anaongea nasi maana yeye njia zake hazichunguziki chukua hatua ya kutengeneza haraka. (Mathayo mt 5:23 -24 Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kasha urudi uitoe sadaka yako). Mungu wetu si wa machafuko anapenda amani, pia kuna sehemu amesema tujitahidi kuitafuta amani tena kwa bidii na huo utakatifu ambao hapana mtu atakaye mwona Bwana asipokuwa nao.

Mbele za Mungu dhambi zote zina msamaha lakini sio dhambi ya kumkufuru (Roho Mtakatifu Marko 3:28 - 29 Amini, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa na dhambi ya milele). Usiwe na hasira iliyopitiliza utampa Shetani mlango wa kukuingia na kukufanyia atakacho, haijalishi kabila lenu mna asili hiyo embu ishinde hiyo asili maana hakuna kisichowezekana. Kabila lako lisikufanye ukaikosa mbingu na nchi mpya, roho hii ya hasira haiwaachagi watu salama na shetani hakatagi tamaa upesi mpaka afanye alichokusudia. Kuwa na hasira si dhambi, dhambi ni pale utakapoikumbatia mpaka ikapelekea kuzaa matunda. Kaini aliambiwa na Mungu dhambi inakutamani lakini yakupasa uishinde.(Mwanzo 4: 7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibari? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.)

Ukiwa hujasamehe unatembea, hujatengeneza na Mungu wako unaweza sababishia wengine madhara, kama ilivyotokea kwa Nabii Yona kusababishia wenzake kupoteza mali na usumbufu katika Safari yao toka Ninawi mpaka Tarshishi (Yona 1:5 Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi) Nabii Yona kesi/hasira yake na Mungu ilipelekea abiria wenzake  na pia kwa kuwa roho ya hasira  haikufanyiwa kazi kikamilifu ilipelekea umauti kutokea mapema. (Yona 4:4-8 Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika…) shetani hamwogopi mtu yeyote hakumwogopa Yesu wewe ni nani? Musa mtumishi wa Mungu aliyefanya mambo makubwa katika historia ya wana wa Israeli. Alikuwa na roho ya hasira iliyojificha ambayo hakuifanyia kazi Kutoka 2:11-15 Musa alivyompiga Mmisri na kukimbia …hasira hiyo aliendelea nayo ikapelekea kumkosesha kuigia mji wa Kaanani pamoja na kuwa aliuona mji kwa mbali. (Hesabu 20:8 Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao) Kitendo cha Musa kufanya kinyume cha maelezo ya BWANA hasira zikamponza. Hesabu 20:9-12 Watu wenye hekima huwa wanashauri kama una hasira si vizuri kufanya jambo wala hata kuongea ni heli ukae kimnyaa kwa muda kabla ya maamuzi. Baada ya kifo cha Musa Mungu alindaa mtumishi mwingine ili kuwawezesha wana wa Israeli kumaliza safari.

 

Maandiko kuna sehemu yanakiri kuwa unaweza kuishika torati yote vizuri lakini ukiikosea katika moja ukawa ukekosa juu ya yote kwa hiyo tujitahidi iwe maombi yetu ya kila siku kushinda huu udhaifu tuishitaki mbele za Mungu mtakatifu kwa kuwa yeye ana nguvu kuliko shetani tutashinda sababu aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliyeko katika dunia.

Kutosamehe kunachafua roho yako, unaweza kuikosa Mbingu au Baraka mbali mbali toka Kwa Mungu.

Malaika ni wajumbe, watumishi wa Mungu wanapotumwa kwako kukuletea baraka tofauti tofauti mbali mbali sababu wenyewe wapo katika roho wanapo kuja wanaiona roho yako imechafuka basi wanarudisha kile kitu walichokuletea wanaenda kukihifadhi kinakaa kilipotolewa, kwa duniani hifadhi hizo tungeweza kuiita kabati, friji, store mpaka utakapo kaa sawa sawa etc. ni kama vile wewe ni mzazi unakuja kwa mwanao mdogo unatamani kumpa kitu kizuri, lakini ukute amejinyea, je utampa kile kitu kizuri, si utaondoka na kumpa siku nyingine au atakapokuwa amejisafisha au amesafishwa.

Mungu hawasikilizi wenye dhambi maombi yao ni kelele

 (Yoh mt 9:31 Twajua ya kuwa Mungu awasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kufanya mapenzi yake, humsikia huyo) sifa zao kwa Mungu huonekana kama ni makelele.

Migogoro mingi katika ndoa chanzo kikubwa ni kutosameana Mume na mke, mhhhhh.Kunyimana nyimana vitu vilivyo haki katika ndoa, kukomoana. Mwanamke& Mwanaume kunyemelewa na Shetani kuhusu kutafuta mbadala  (Mpumbavu huamua kwa haraka na, madhara yakamkuta) Shetani anazunguka zunguka akitafuta mtu awe mwanachama  mapepo nayo yanazunguka zunguka hayalali. (1Pet 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka zunguka akitafuta mtu ammeze).

 

WATUMISHI WACHACHE WALIOKIMBILIA TOBA BAADA YA KUGUNDUA KUWA WAMEKOSEA

        i.            Daudi kwenye kesi ya Mkewe na Uria 2Samweli 12:13

      ii.            Petro alivyomkana Yesu mara tatu kuwa hamjui Yohana mt 18:25-27 Baada ya hili tukio hatumuoni Ptro akiomba msamaha kwa ajili ya tukio hili alilolifanya la kumkana Yesu mara tatu (Yohana mt 21:15 Basi walivyokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni wa Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?Akamwambia, Naam, Bwana , wewe wajua kuwa nakupenda.Akamwambia lisha wana kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia Ndiyo Bwana wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.) Pamoja na kuwa Petro alikasirika bila kujua Yesu alikua anamfungulia kifungo chake kutokana na kumkana Yesu mara tatu kwake baada ya kukiri kwa kinywa chake akawa amepona.                                                                                                                                                                                  

 

 

BAADHI YA MATATIZO/ ATHARI ANAZOWEZA KUPATA ALIYE NA ROHO YA KUTOSAMEHE/KUWEKEZA

Mioyo yetu haikuumbwa ikae na uchungu, hasira, chuki. Ukikaribisha vitu hivyo unakaribisha Magonjwa, k.v. PreshaMsongo wa mawazoKichwa KuumaVidonda vya TumboKuchanganyikiwa (Kuongea Peke yako),  Ajari, Asilimia kubwa ya watu wanaojinyonga, kunywa sumu ni watu walioumizwa na uchungu uliopitiliza Yusufu baada ya kuonana na ndugu zake walio muuza alikumbuka mabaya aliyo tendewa, uchungu ukamjia akaomba aondolewe kila mtu ili aweze pata faragha ya kulia, kulia nako ni dawa kunasaidia kutoa uchungu wa moyoni,  baadhi ya watu wanasema kama mtu hatalia katika matukio mbali mbali yanayotukuta wanadamu anaweza kupata matatizo fulani ya kiafya, kwa hiyo kulia kunasaidia kutoa sumu na kupunguza baadhi ya magonjwa.

(Yuda Iskariote Mt 27:5), Watu wengine wamekasirika wakajikuta wapo Kifungoni wanajuta.Petro hakuwekeza kosa alilotenda la kumkana Yesu tena mara 3 alitubu na kuomba msamaha, Akasamehewa. Naamini hata Yuda pamoja na kumsaliti Yesu kama angekuwa na roho ya toba angeweza kusamehewa. Ila binadamu tuna tofautiana tabia tunaweza kuwa hata mapacha lakini tusifanane kila kitu. Ila tuwe na moyo wa toba, toba na kunyenyekea na kurudi kwa mwenyezi Mungu na kutotubu ni roho ya kiburi. Na Mungu huwapinga wenye kiburi (1Petro 5:5 Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee.Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi,lakini huwapa wanyenyekevu neema.)

 

Kwa kawaida kati ya watu wawili waliokoseana  anayesamehe na anayesamehewa anayeumia zaidi ni yule asiye samehe, sababu kila ukimwona mgomvi wako unakumbuka wakati labda mwenzako alisha samehe, na kusahau siku nyingi, kwa hiyo usiposamehe ndio unaumia zaidi. 

Sala Ya Bwana Tunakiri kuwa “Baba yetu uliye Mbinguni, utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe Waliotukosea” Tunajifunga kwa maneno ya kinywa chetu wenyewe. Kama hutaki kusamehe na kuachilia na Mungu naye hakusamehi ng’o nani anayeweza kuishi bila msaada wa Mungu, bila ulinzi wake, upendo wake, neema yake? Ukihukumiwa kwa kosa hilo siku ya siku ni haki yako sababu umekiri kwa kinywa chako mwenyewe.

Tuwe wepesi wa kuomba msamaha kwa Mungu wetu, wenzi wetu hata watoto wetu, majirani, wafanyakazi wenzetu n.k

Katika wanafunzi aliokuwa nao Yesu, Yuda alimsaliti Yesu akakaa na uchungu hakuutoa ukamdhuru , Petro naye alimsaliti Yesu tena mara tatu. Yuda mara moja, Petro alimkana Yesu mara tatu akatubu fasta. Akapata msamaha, sio suala la dhambi kubwa au ndogo Mungu kwake hata dhambi iwe nyekundu husamehe kabisa. Mungu wetu aliyeumba mbingu na nchi yupo mbali sana, lakini kwa uwezo wake yupo pia karibu sana mwombe yeye akuwezeshe kusamehe, kwa nguvu zako peke yako huwezi. Yeye ni wa huruma,na rehema na anatuvumilia kwa mengi atakuwezesha, maana hakuna jambo lililo gumu la kumshinda yeye Mungu.

Tena pia tunaaswa tukiwa na hasira sana au furaha sana tusiamue jambo, maana ni rahisi sana kuamua kinyume na mapenzi ya Mungu (Mat 14:6-7 Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode,binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote, atakaloliomba.) Wakati Bwana Yesu alipokuwa anaelekea Kalvali kuna kipindi alikuwa anadhalilishwa, Yeye akiwa mwana wa Mungu ambaye Mungu amependezwa naye aliulizwa swali akiwa na maumivu, alinyamaza kimnya, tujifunze kuwa wakati mwingine kuna uponyaji katika kutojibu jibu au kukaa kimnya. (Mark 15: 4 -5 Pilato akamwuliza tena akisema,Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.)

 

 

Stephano Alipigwa na vijana waliofundishwa na Sauli Stephano” Alikufa huku akimwomba Bwana Usiwahesabie Dhambi hii, wasamehe Bwana. (Mdo 7:60 Alipiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii.Akiisha kusema haya akalala). Hapa kulala maana yake ni kufa.

 

Bwana Yesu pamoja na kudhalilishwa yeye akiwa kama Mwana wa Mungu alikuwa na Jeshi kubwa la Malaika ambalo angeweza kuliamlisha lifanye vyovyote, likafanya alidhalilishwa lakini akasema, "Bwana wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo".

 

Yusufu pamoja na kuwa ndugu zake walikuwa hawampendi na visa kede kede ikiwemo kumuuza ugenini lakini siku zikapita wakiwa na njaa walikimbilia kwa Yusufu wakihitaji msaada wa chakula wasife kwa njaa,  Yusufu aliwajua ndugu zake lakini wao hawakumjua, aliwatendea mema nduguze.  

Habari ya Yusufu pia itufundishe jambo jingine hapa, kitendo cha Yusufu kutokasirika kutochukua maamuzi magumu mf.kujiua kwa mabaya aliyotendewa na ndugu zake, kwake ilikuwa ni mtihani ambao kushinda kwake imempelekea kuwa Waziri mkuu. Je wewe unajua baada ya jaribu au mtihani huo Mungu ameandaa nini mbele yako? Kwa nini ukubari mwovu akuharibie na kuvuruga lile jema ambalo Mungu alikupangia ulipate ukiwa hapa duniani, kabla ya yeye mwenyewe hajahitimisha uhai wako? Hivi unajua kusudi la Mungu kukuleta, kukuweka hapa duniani? Kila Mtu aliyepo hapa duniani yupo kwa kusudi fulani la ki Mungu, ndo maana utakuta wanaokufa sio kwamba wana madhambi sana  kuliko sisi tunaoendelea kupumua.                                                                                                                                                     

 

Eliya alifanyaje ? Kama Eliya aliweza kuagiza moto kutoka Mbinguni uteketeze 50 Yesu si Zaidi! Eliya Mtu wa Mungu kama mimi, kama wewe tu wewe je?  2 Wafalme 1:10 Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka ukamteketeza, yeye na hamsini wake)

 

Kutoomba Toba ni kiburi mbele za Mungu au wanadamu, maandiko yanasema Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa neema wanyenyekevu.sio hivyo tu lakini pia kusamehe ni kutii agizo la Mungu, (Warumi 12:19 Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.)

Ukilipa kisasi unapingana na agizo la Mungu yaani huamini kuwa Mungu atafanya alichoahidi, yaani unamfanya kuwa Mungu ameahidi uongo hutaki Mungu akupiganie unajipambania mwenyewe.

(Mithali 17:13 Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani  mwake). Maandiko yanaposema mabaya hayataondoka nyumbani mwake maana yake, nyumbani mwako inaweza ikawa ni kwenye biashara yako, kazi zako, ndoa yako, watoto wako, yaani kwa ufupi ni kwenye vitu vinavyokuhusu. Hilo ni neno la Mungu na neno la Mungu ni kweli na amini.

Sio kwa sababu maandiko yanasema Samehe saba mara sabini basi ndo iwe tiketi ya  wewe kukosea kwa makusudi , sababu utasamehewa kwa hiyo ukaamua kuleta Makwazo ya makusudi. Maandiko yana onya juu ya mtu kama huyo aletaye makwazo. Pia sio kwa sababu Mungu ni wa huruma au anasemehe si mwingi wa hasira, tusijiachilie sana tuwe na tahadhari.

 

(Luka 17. 1 Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!)

 

Hata mtu akiamua kumpa Yesu maisha yake, sio kigezo cha kutopata makwazo, makwazo yapo na hayataisha mpaka mwisho wa dunia, inapasa tuyashinde, maana ndio njia ya msaraba hiyo, hakuna njia ya mkato, Yesu alipitia wafuasi wake lazima nao wapitie. 

 

Kama utakuwa umetendewa neno ovu nawe ukaamua kulipa kisasi, hapo utakuwa ukifanya kitu kinaitwa Kuhukumu,   maandiko yanasema usihukumu, usije ukahukumiwa, kisasi ni jukumu au kazi ya  Mungu mwenyewe atalipa. (Mathayo 7:1 Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi)

 

 

(Waefeso 4:26-27 '' Mwe na hasiraila msitende dhambijua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka ; wala msimpe ibilisi nafasi.)

 

Shetani hawezi kukushambulia mpaka umfungulie Mlango kupitia uovu hasira ni Mlango mmojawapo anaotumia kushambulia, ili shetani apate nguvu na uhalali wa kukushambulia wewe kama mwana wa Mungu lazima umvutie, utamvutia kwa kuwa na uwepo wa dhambi moyoni mwako. Ndo Maana kama ni msomaji wa biblia utagundua pia wakati Yesu alipokuwa akiwaombea, akiwafungua baadhi ya watu alikuwa akiwaambia umekuwa mzima "Usitende dhambi tena" (Yoh 5:14

Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya Hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi) Na sababu nyingine inayofanya watu wengi leo kushindwa kusamehe ni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu ndani yao pia hawataki kuomba msaada wa Roho Mtakatifu,  Roho Mtakatifu akiwa ndani yako matunda yake yataonekana tu hayajifichi. Na roho ya shetani ikitawala ndani yako matunda yake yataonekana tu hata ujifiche vipi. Katika maandiko yanakiri kinywa cha mtu hunena yale yaujazayo moyo wake (Luka Mtakatifu 6:45 Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya mwili wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake).

 

Kisasi ni cha Mungu, yeye atalipa, tena wakati mwingine Mungu hulipa tangia hapa duniani, Duniani tunapita hatuishi milele sisi ni kama maua ya kondeni.

 

 

Abigaili, mwanamke mwenye hekima wa Israeli Agano la kale, anatuwekea kielelezo kinachoonyesha matokeo ya kuomba msamaha, ingawa aliomba msamaha kwa kosa la mumewe. Alipokuwa akiishi nyikani pamoja na watumishi wake, Daudi, aliyekuja kuwa mfalme wa Israeli, alilinda kondoo za Nabali, mume wa Abigaili. Hata hivyo, wakati vijana hao wa Daudi walipoomba mkate na maji, Nabali aliwafukuza na kuwatusi vibaya sana. Daudi alikasirika na kuongoza wanaume 400 hivi kwenda kumpiga Nabali na nyumba yake. Alipojua habari hiyo, Abigaili alifunga safari kwenda kumlaki Daudi. Alipomwona, Abigaili alimwangukia miguuni pake na kusema: “Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.” Kisha Abigaili akaeleza hali ilivyokuwa na kumpa Daudi zawadi ya chakula na maji. Ndipo Daudi akamwambia: “Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.”—1Samweli 25:2-35. Baada ya siku 10 Nabali alifariki, alivyofariki Daudi alifanya mpango wa kumuoa Abigaili (Malipo ni hapa hapa Duniani)

 

 

Solomoni Mukubwa (Ushuhuda)

Yeye ni Raia wa Kongo anayeishi Kenya ni mtoto wa kwanza katika familia yao baba yao alipoongeza mke mwingine Huyo mke Mwingine alimloga Solomoni Mukubwa alipokuwa na umli wa Miaka 12 akawa na uvimbe ambao ulipelekea kukatwa kwa mkono wake ili kunusuru uhai wake, aliangaikiwa sehemu nyingi na wazazi wake bila mafanikio. Alijua kuwa amelogwa na mama yake wa kambo baada ya yeye mwenyewe kukiri kuwa alifanya hivyo. Huyu mama wa kambo naye aliokoka baada ya yeye naye kupata pigo ‘Mwanawe alirukiwa na kijiti cha moto jichoni kilichopelekea jicho la mwanawe kuharibika kabisa

(Malipo ni  hapa hapa Duniani) Solomoni Mukubwa katika kumbukizi ya tukio alilowahi kupitia ameimba wimbo unaitwa nimewasamehe !!!

 

Usipende kuudhi watu ovyo ovyo watu wengine Wanampendeza Mungu kiasi ambacho ukikorofishana nao Malaika wananunua ugomvi unashangaa tu, unapata pigo hujui chanzo ni nini pigo inaweza kuwa gonjwa fulani, ajari au hata kifo kwa sababu zisizokuwa na majibu,sio watu tu kuna baadhi ya mataifa pia ukiyagusa umegusa mboni ya jicho la Mungu, unapigana nao bila kujua kuwa nyuma ya mtu au Taifa husika yupo Mungu. Hata katika ufalme wa giza nao kama kuna kufanana Fulani ukimfanyia kitu kibaya anayelindwa na majini unaweza kukuta majini wanakushambulia hata kukuua kabisa. Hata katika ulimwengu wa mwili wa wanasiasa sio vizuri kumsema kwa kumzalilisha mtu mwenye cheo mf.Rais wa nchi unaweza kushambuliwa na watu usio wajua, ukaingia matatizoni, kuwa makini chunga ulimi wako ndugu yangu kaka au dada. (1Petro 3:10 Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya,)

 

Kaini na Habili

Kisa cha Kaini kumuua Habiri ni hasira, uchungu ambao haukutubiwa (Mwanzo 4:3-15 Ikawa hatimaye Kaini aleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA.Habiri naye akaleta mazao ya kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabari Habiri na sadaka yake ; …)Ukiwa na hasira au uchungu moyoni mwako hata Sadaka yako haitapokelewa mbele za Mungu ...(Mathayo 5:23 -24 Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako). hata Maombi yako Mungu hayasikilizi sababu Mungu hawasikilizi wenye dhambi. 

Kuna watu tunaishi nao hapa duniani ni wagumu mno kusamehe wenzao, hata umwombe msamaha yeye atang'ang'ana na msimamo wa kutosamehe, watu wa jinsi hii unatakiwa ujiepushe nao maana wanaishi chini ya laana hawatafanikiwa ng'o hata kama wanamafanikio basi mafanikio yao yatakuja kupotea ghafla , Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, mshahara wa dhambi ni mauti.

 

uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.(Waefeso 4:31,32)

 

Tuuangalie msaraba ili tushinde, dunia yote imejaa makwazo, hata Yesu alisema " ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo mimi nimeushinda ulimwengu" (Yohana Mtakatifu 16:33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu.Ulimwenguni mnayo dhiki ; lakini jipeni moyo ; mimi nimeushinda ulimwengu.)

 

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo,

Vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

      1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).
      2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike 5:17)
      3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa linalokili
        wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
                   (Waebrania 10:25).

4. Fanya kazi kwa bidii na uaminifu,jitume usione aibu, acha uvivu, tafuta pesa, Mungu katoa agizo tangu kale,Yeye alifanya kazi, Yesu alifanya kazi, mitume vivyo hivyo ( 2Thesalonike  3:10)

         5.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na (1Petro 5:8).
         6.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu, huwezi kujua nani
                       anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).